Na Hassan Mwasha, Gazetini
MOJA ya hatua kubwa zilizopigwa na Shirika la Reli nchini (TRC) ni kuondokana na utegemezi kwa Serikali, ambapo katika Mwaka wa Fedha wa 2026-27 litaanza kujitegemea katika ulipaji wa mishahara ya waajiriwa wake.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, akiwasilisha Bajeti hiyo Mei 13, 2026 Bungeni mjini Dodoma, akisema: Mheshimiwa Spika, Wizara inaishukuru Serikali kwa kuchukua hatua za kuboresha Shirika la Reli Tanzania (TRC), zoezi lililoanza mwaka 2017.
“Tangu kuanzishwa kwa Shirika hili, Serikali imekuwa ikitoa ruzuku ya mishahara. Naomba kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa, katika mwaka 2026/27, TRC haitatengewa tena ruzuku kwa ajili ya mishahara kutoka Serikalini.”

SGR YAZIDI KUCHANJA MBUGA
Katika hotuba yake, Waziri Mbarawa amesema Serikali kupitia TRC imeendelea na ujenzi na uendeshaji wa reli ya SGR pamoja na kuboresha mtandao wa reli ya MGR yenye urefu wa takribani kilometa 2,707.
“Ujenzi wa reli ya SGR unatekelezwa kwa awamu mbili, ikihusisha kilometa 1,219 za njia kuu kwa awamu ya kwanza kutoka Dar es Salaam – Mwanza; na kilometa 1,590 za awamu ya pili, ikijumuisha vipande vya Tabora – Kigoma na Uvinza – Musongati,” amesema.
Aidha, Waziri Mbarawa amesisitiza kuwa kukamilika kwa awamu hizo mbili za reli ya SGR kutaifanya Tanzania kuwa na mtandao wa jumla ya kilometa 2,809 za reli ya SGR.
Wakati huo huo, Serikali kupitia TRC imeendelea na ujenzi wa Reli ya SGR, ambapo hadi kufikia mwezi Machi, 2026 ujenzi wa kipande cha kwanza Dar es Salam – Morogoro (km 300) na kipande cha pili Morogoro – Makutupora (km 422) umekamilika kwa sehemu kubwa.
“TRC inaendelea na utoaji wa huduma ya usafiri wa treni kwa vipande husika. Kwa kipande cha Mwanza – Isaka (km 341), ujenzi unaendelea na umefikia asilimia 68.77.
“Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwezi Machi 2026, ujenzi wa reli ya SGR katika kipande cha tatu: Makutupora – Tabora (km 368) na kipande cha nne: Tabora – Isaka (km 165) unaendelea,” amesisitiza Waziri Mbarawa.
Ameongeza kuwa ujenzi wa vipande viwili hivyo ulikuwa na changamoto zilizosababisha utekelezaji wake kuwa na kasi ndogo.
Hata hivyo, Serikali tayari imepata suluhisho la kukamilisha ujenzi wake kwa kupata mkopo wenye masharti nafuu wa thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.277, sawa na takriban Sh trilioni 3.32.
ONGEZEKO USAFIRISHAJI WA ABIRIA, MIZIGO
Waziri Mbarawa ameeleza kuwa Serikali kupitia TRC imeendelea na usafirishaji wa abiria kati ya Dar es Salaam na Dodoma kupitia reli ya SGR.
“Usafirishaji kupitia reli hiyo umezidi kuimarika ambapo katika kipindi cha Julai, 2025 hadi Machi, 2026, jumla ya abiria milioni 2.51 walisafirishwa, ikilinganishwa na abiria millioni 2.05 katika kipindi kama hicho kwa mwaka wa fedha 2024/25, sawa na ongezeko la asilimia 22.40,” amesema.
Anaongeza pia, katika kipindi cha kuanzia Julai, 2025 hadi kufikia mwezi Machi 2026, TRC ilisafirisha jumla ya tani 102,452 za mizigo, ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Serikali ya kuanza usafirishaji wa mizigo kupitia reli ya SGR.
Katika hatua za kuunganisha miundombinu ya reli ya SGR na MGR, Serikali imeendelea na uunganishaji wa reli hizo katika eneo la Ruvu ili kuwezesha usafirishaji wa mizigo kutoka Bandari za Dar es Salaam na Tanga, ambapo utekelezaji wake umefika asilimia 85.
“Aidha, ujenzi wakuunganisha reli za MGR na SGR unaendelea katika eneo la Bahi kwa lengo la kuwezesha uhamishaji wa mizigo (transhipment) kati ya reli hizo 2 na unaendelea vizuri.
“Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuboresha Reli ya MGR kwa kubadilisha reli nyepesi na kuweka nzito, pamoja na kuongeza uwezo wa madaraja. Ukarabati huo unaendelea kupitia Mfuko wa Reli, ambapo hadi Machi 2026, kipande cha Kaliua–Mpanda kilikuwa kimekamilika kwa asilimia 32.72,” amesema.
UDHIBITI WA MAFURIKO
Kwa upande mwingine, Waziri Mbarawa amesema katika kukabiliana na mafuriko yanayoathiri Reli ya MGR katika eneo la Kilosa–Kidete–Igandu, Serikali imekamilisha ujenzi wa njia ya reli yenye urefu wa km 6.2 na daraja katika eneo la Godegode–Gulwe, ambapo ujenzi umefikia asilimia 99.
Hatua hiyo inakwenda sambamba na maandalizi ya ujenzi wa mabwawa sita (Kidete, Kimagai, Buigiri, Ikowa, Hombolo na Dabalo) katika Mto Kinyasungwe ili kupunguza mafuriko na kuboresha uendeshaji wa reli.
CHANGAMOTO RELI YA TAZARA
Licha ya Serikali ya Tanzania na Zambia kuendelea kushirikiana katika kusafirisha mizigo na abiria kwa kutumia Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), changamoto kubwa ni ufanisi mdogo unaotokana na uchakavu wa miundombinu na uhaba wa vitendea kazi.
Katika hilo, Waziri Mbarawa anaibua matumaini mapya akisema nchi hizo zilisaini mkataba wa uendeshaji (Concession Agreement) na Kampuni ya CCECC, lengo likiwa ni kuboresha reli ya TAZARA.
“Kampuni hii itawekeza jumla ya Dola za Marekani bilioni 1.4, ambayo ni sawa na takriban Shilingi trilioni 3.6. Maboresho ya reli hii yanatarajiwa kuongeza uwezo wa kusafirisha mizigo milioni 2.4 kwa mwaka na kuzalisha ajira mpya 100,000,” anaeleza Waziri Mbarawa.


