LOS ANGELES, Marekani
ACHANA na milionea. Sahau pia kuhusu bilionea. Mfanyabiashara maarufu wa Marekani, Elon Musk, amekuwa trilionea kwa kwanza hapa duniani.
Musk amefikia hadhi hiyo baada ya mafanikio makubwa ya kampuni yake ya teknolojia ya SpaceX na sasa utajiri wake ni Dola za Marekani trilioni 1.11.
Kwamba amewazidi matajiri wote, wakiwamo wamiliki wa Google, Larry Page na Sergey Brin, bosi wa Amazon, Jeff Bezos, na mmiliki wa kampuni ya LVMH, Bernard Arnault.
Kwa utajiri wake wa sasa, Musk amemzidi Larry Page kwa Dola bilioni 700. Page anayeshika nafasi ya pili, ana utajiri wa Dola bilioni 294, akifuatiwa na Brin (Dola bil. 271), Bezos (Dola bil. 249).
Alianza biashara ya teknolojia katika miaka 1990 na kufikia Januari, 2020, alikuwa nafasi ya 35 kwenye orodha ya matajiri duniani, wakati huo akimiliki Dola bilioni 28.
Musk, mbali ya kuwa na asilimia 12 ya hisa kwenye Kampuni ya magari ya umeme ya Tesla, pia anamiliki mtandao wa kijamii wa Twitter alioununua mwaka 2022.
Kwa hesabu rahisi, trilioni moja ni sawa na bilioni 1,000. Ni sawa pia na milioni moja ziwe milioni moja. Ndiyo utajiri wa Musk kwa sasa.
Ni kiasi cha pesa kinachotosha bila wasiwasi wowote kugharamia safari ya wanasayansi kwenda na kurudi mwezini mara 200.
Pia, ni fedha zinazotosha kumpa kila binadamu aliye duniani kwa sasa Dola 122 (Sh 319,523 za Tanzania). Kwa mujibu wa takwimu za Sensa ya Marekani, dunia ina watu bilioni 8.2.
Vilevile, trilioni 1.11 za utajiri wa Musk zinatosha kujenga nyumba milioni 2.5 nchini Marekani. Bei ya nyumba nchini humo, kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni, ni Dola 403,200.
Wakati huo huo, wakati huu bei ya gesi ikiwa juu duniani kote, trilioni 1.11 alizonazo Musk zinatosha kununua vidumu bilioni 243. Kwa sasa, bei ya kidumu cha gesi kwa kidumu kimoja ni Dola 4.11.



