Na mwandishi wetu, Gazetini
KAMPUNI ya Airtel Africa imeendelea kuimarisha mchango wake katika maendeleo ya kijamii, kiuchumi na mazingira barani Afrika baada ya kuongeza upatikanaji wa huduma za mawasiliano, huduma za kifedha kwa njia ya simu na matumizi ya nishati safi, hatua zilizosaidia kufungua fursa kwa mamilioni ya wananchi katika nchi 14 inazohudumia ikiwemo Tanzania.
Hayo yamebainishwa katika Ripoti ya Maendeleo ya Airtel Africa ya mwaka 2026 iliyotolewa Juni 10, 2026, ikionesha mafanikio yaliyopatikana katika mwaka wa fedha 2025/26 kupitia uwekezaji katika miundombinu ya kidijitali, ujumuishaji wa kifedha na utekelezaji wa mikakati ya uhifadhi wa mazingira.
Ripoti hiyo inaonesha kuwa Airtel Africa imeendelea kupunguza pengo la kidijitali kwa kuongeza upatikanaji wa huduma za mawasiliano hususan katika maeneo ya vijijini, huku ikiimarisha matumizi ya teknolojia za kidijitali zinazochochea ukuaji wa uchumi na upatikanaji wa huduma muhimu kwa wananchi.
Akizungumzia mafanikio hayo, Mtendaji Mkuu wa Airtel Africa, Sunil Taldar, amesema upatikanaji wa mawasiliano, huduma za kifedha na elimu ya kidijitali umeendelea kuwa nyenzo muhimu ya kufungua fursa za maendeleo kwa mamilioni ya Waafrika.
“Barani Afrika, upatikanaji wa mawasiliano, huduma za kifedha na elimu ya kidijitali unazidi kuwa muhimu katika kufungua fursa za kiuchumi. Airtel Africa inaendelea kupanua huduma hizi kwa mamilioni ya watu, hususan katika maeneo ya vijijini na yale ambayo bado hayajafikiwa kikamilifu,” amesema Taldar.
Amesema kampuni hiyo imeendelea kupanua mtandao wake, kuongeza matumizi ya simu janja na kuimarisha huduma za Airtel Money sambamba na kuwekeza katika matumizi bora ya nishati ili kuboresha ufanisi wa shughuli zake.
“Kwa kuboresha matumizi ya nishati na kupunguza utegemezi wa dizeli, tunaimarisha ufanisi na ustahimilivu wa shughuli zetu huku tukichangia ukuaji endelevu wa biashara na jamii,” amesema.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, upatikanaji wa huduma za mtandao wa simu umefikia asilimia 81.9 mwaka 2025/26 kutoka asilimia 81.2 mwaka uliotangulia, huku upatikanaji wa huduma hizo katika maeneo ya vijijini ukiongezeka hadi asilimia 73.1 kutoka asilimia 72.2.
Ripoti hiyo pia inaonesha kuwa matumizi ya simu janja yameongezeka hadi asilimia 49.5 kutoka asilimia 44.8 mwaka uliopita, hali inayowezesha wananchi wengi zaidi kupata huduma za mtandao, elimu na majukwaa mbalimbali ya kidijitali.
Katika eneo la ujumuishaji wa kifedha, Airtel Money imeendelea kupanua huduma zake kwa kasi ambapo idadi ya wateja imeongezeka kutoka milioni 44.6 hadi zaidi ya milioni 54 ndani ya mwaka mmoja.
Aidha, thamani ya miamala iliyochakatwa kupitia Airtel Money imefikia takribani dola za Marekani bilioni 196, ikilinganishwa na dola bilioni 136 mwaka uliopita, huku asilimia 44.1 ya watumiaji wa huduma hiyo wakiwa wanawake.
Ripoti hiyo imeeleza kuwa ongezeko la mawakala wa Airtel Money kutoka milioni 1.7 hadi milioni 2.4 limeendelea kuchochea ajira, ujasiriamali na upatikanaji wa huduma za kifedha katika maeneo mengi ya Afrika.
Katika sekta ya elimu, Airtel Africa imeendelea kuimarisha upatikanaji wa teknolojia mashuleni kupitia ushirikiano wake na UNICEF. Kufikia Machi 31, 2026, jumla ya shule 3,043 zilikuwa zimeunganishwa na huduma za intaneti bila malipo, kutoka shule 2,176 mwaka uliotangulia.
Kwa upande wa mazingira, kampuni hiyo imeendelea kuchukua hatua za kupunguza athari za shughuli zake kwa mazingira kwa kuongeza matumizi ya umeme wa gridi ya taifa na kupunguza utegemezi wa nishati ya dizeli.
Ripoti inaonesha kuwa zaidi ya vituo 950 vya miundombinu ya kampuni vilihamishwa kutoka matumizi ya nishati isiyounganishwa na gridi ya taifa kwenda kwenye umeme wa gridi, ikilinganishwa na vituo 500 mwaka uliopita.
Hatua hiyo imewezesha kupunguzwa kwa matumizi ya dizeli kwa lita milioni 9.1 katika kipindi cha mwaka mmoja, huku asilimia 94 ya taka zote zilizozalishwa na kampuni zikirejelewa, kutoka asilimia 93 mwaka 2024/25.
Ripoti hiyo imeandaliwa kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya Global Reporting Initiative (GRI) pamoja na miongozo ya sekta ya mawasiliano ya simu ya GSMA, ikionesha dhamira ya Airtel Africa ya kuendeleza uwajibikaji, uwazi na maendeleo endelevu katika shughuli zake.
Kwa sasa, Airtel Africa inahudumia zaidi ya wateja milioni 183.5 katika nchi 14 za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, ikiwa na lengo la kuendelea kukuza ujumuishaji wa kidijitali na kifedha ili kuboresha maisha ya wananchi na kuharakisha maendeleo ya uchumi wa Afrika.


