24.4 C
New York

Mpasuko ndani ya uongozi wa Iran?

Published:

TEHRAN, Iran

LENGO ni moja tu, kuhakikisha dunia inatambua na kuheshimu nguvu ya Iran, hasa dhidi ya Marekani na washirika wake, ikiwamo Israel. Katika hili, viongozi wa Iran wako pamoja.

Lakini, bado uongozi wa juu ya Taifa hilo la Mashariki ya Kati wanatofautiana katika jambo moja. Namna ya kukabiliana na Marekani.

Iko hivi; ndani ya uongozi, lipo kundi lisilotaka hata kusikia suala la mazungumzo na Marekani. Halioni sababu ya kukaa mezani na maadui zao na liko tayari kuona vita vikiendelea hata kwa miaka mingi ijayo.

Kwa mujibu wa taarifa, kundi hilo, licha ya uchache wa wafuasi, lina nguvu kubwa ndani ya uongozi, ikiwamo ya kiuchumi. “Wana pesa. Wana nguvu sana,” anasema Vali Nasr, mchambuzi wa siasa za Ukanda wa Mashariki ya Kati kutoka Chuo Kikuu cha Johns Hopkins.

Kwa upande mwingine, kundi linalomuunga mkono Rais Masoud Pezeshkian, na Spika wa Bunge, Mohammad Bagher Qalibaf, linapingana na mtazamo huo, na badala yake linaamini katika mazungumzo.

Na itakumbukwa, Qalibaf alikuwa mstari wa mbele katika awamu zote za mazungumzo na Marekani, yakiwamo yaliyofanyika Pakistan miezi michache iliyopita.

Hoja ya kundi hilo linaloongozwa na mshauri wa Qalibaf, Mahdi Mohammadi, ni kwamba mazungumzo ndiyo silaha sahihi zaidi, kuliko kuendelea kuumiza uchumi wa Taifa lao kwa mapigano yasiyo na siku rasmi ya kumalizika.

Wakati makundi hayo yakiripotiwa kuwa kwenye msuguano huo, Kiongozi mpya wa Iran, bado haijafahamika Ayatollah Mojtaba Khamenei anasimama upande upi.

Ni muumini wa vita au mazungumzo? Licha ya kutokueleza msimamo wake, kila kundi linadai kuungwa mkono na kiongozi huyo.

Tangu alipojeruhiwa katika shambulizi la kwanza lililomuua baba yake Februari 28, 2026, Khamenei ameendelea kuishi mafichoni.

Kwa upande mwingine, mpasuko huo ndani ya uongozi inaibua swali jingine la msingi, kwamba ipi hatima ya Iran baada ya kumalizika kwa vita vyake na Marekani? Itaanza vita ya makundi hao?

Related articles

Recent articles