NAYPYIDAWA, Myanmar
KWA wananchi wa Myanmar, siasa zinawapitisha katika ukurasa mpya uliojaa machungu ya kukimbia nyumba na familia zao ili kujinusuru na utawala wa kijeshi nchini humo.
Kwa sasa, wengi wao wanaishi kama wakimbizi mjini Mae Sot, Thailand, ambako huko walau wanapumua, licha ya kwamba bado wana kiu ya kurudi nyumbani na kuungana na ndugu, jamaa na marafiki.
Hata hivyo, kurudi Maynmar kwa sasa ni jambo gumu kwao, wakifahamu wazi kuwa bado jeshi linaongoza Serikali tangu lilipofanya mapinduzi yaliyopingwa kwa maandamano makubwa ya raia mwaka 2021.
Maandamano hayo ambayo hata hivyo yalizimwa na jeshi, huku mamia walifariki, maelfu wakijeruhiwa, na wengi walikamatwa na kuhukumiwa vifungo vya gerezani.
Mapema mwaka huu (2026), uliofanyika Uchaguzi lakini vyama vikubwa vya upinzani vilizuiwa kushiriki ili kumpa nafasi kiongozi wa kijeshi, Jenerali Min Aung Hlaing, kushinda na kuidanganya dunia kuwa amechaguliwa na raia.
Wengi hawakuutafsiri kuwa ni Uchaguzi, bali ‘uchafuzi’ na ‘kiini-macho’ cha kuzika kivuli cha Rais aliyeondoshwa kwa mapinduzi, Aung San Suu Kyi.
Maisha ya raia wa Myanmar wakiwa Mae Sot ni ya kujificha kwa kushinda ndani, wakihofia kukamatwa na polisi wa Thailand kwani wengi wao hawana vibali vya kuishi nchini humo.
Wengi waliingia kwa kuvuka Mto Moei, ambao unazitenganisha nchi mbili hizo. Mmoja ya maofisa wa zamani wa jeshi la Myanmar, ambaye baadaye alihamia upinzani, anasema amekuwa akitoka nje mara mbili tu kwa mwezi.


