LUSAKA, Zambia
ZAMBIA iko mbioni kuingia katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Agosti, 2026, huku wanaharati wa haki za binadamu wakitilia shaka hali ya uhuru wa kutoa maoni, hasa kwa vyombo vya habari nchini humo.
Licha ya kukiri mabadiliko mazuri mengi tangu Rais Hakainde Hichilema kuingia madarakani mwaka 2021, wanaharakati wa uhuru wa vyombo vya habari wanaona bado kuna changamoto katika mifumo, sheria na shinikizo la kiuchumi.
Kama wanavyolalamika wanasiasa wa upinzani, wanaharakati wanatolea mfano namna vyombo vya habari vya umma vinavyozipa nafasi kubwa taarifa zinazokihusu Chama tawala kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Awali, kiongozi wa Chama cha upinzani cha National Democratic Party, Saboi Imboela, alisema: “Vyombo vya habari vya umma vinapendelea Chama tawala, wakati vyana vya upinzani vimebaki kutegemea vyombo binafsi.”
Kwa upande wake, Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA) vinaona hali ya uhuru wa vyombo vya habari kuimarika nchini Zambia, licha ya changamoto zinazotajwa.
“Vyombo vya habari viko huru kuliko awali, ingawa bado kuna udhaifu,” amesema Mwenyekiti wa MISA nchini Zambia, Kennedy Mbulo, katika mahojiano yake na DW.
Hata hivyo, Mbulo anasema chagamoto za kiuchumi, kutegemea zaidi matangazo na presha za kisiasa vinaathiri kwa kiasi kikubwa uhuru waandishi wa habari.
Aidha, wanaharakati wanaona kipindi cha uchaguzi ni kigumu kwa waandishi, hasa wanaoripoti masuala ya rushwa, uwajibikaji na mikutano ya kampeni.
Costa Mwansa, ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari nchini Zambia, amesema udhaifu wa kiuchumi umezifanya vyombo vingi ‘kujipendekeza’ kwa wanasiasa na kampuni ili kupata matangazo, hivyo kushindwa kusimamia uwajibikaji kwa kuibua taarifa za rushwa.
Lakini, majukwaa ya kidigitali yameoonekana kuwa kimbilio la wananchi wengi, ikizingatiwa kuwa vyombo vya habari vya mkondo-mkuu vya redio, televisheni na magazeti vimeingia kwenye mkwamo huo.


