LONDON, Uingereza
KABLA ya kuanza kwa fainali za Kombe la Dunia za mwaka huu (2026), hawakuwa na majina makubwa, lakini sasa wanawindwa na klabu kubwa za Ulaya baada ya kung’ara kwenye mashindano hayo.
Ni akina nani hao? Ni baadhi ya wachezaji wa timu za soka za mataifa mbalimbali na huenda wakasajiliwa na vigogo majira haya ya kiangazi.
AYYOUB BOUADDI
Kiungo mwenye umri wa miaka 18 wa klabu ya Lille ya Ufaransa na timu ya soka ya Taifa ya Morocco.
Bouaddi alionesha kiwango bora katika mchezo wa kwanza wa Morocco dhidi ya Brazil na tangu akafanya vizuri kwa kipindi chote cha mashindano.
Kwa sasa, Arsenal wanaitaka saini ya nyota huyo, ingawa Lille wanakazania kumbakiza kwa ajili ya msimu ujao wa 2026-27.
GILBERTO MORA
Akiwa na umri wa miaka 17 tu, kiungo huyo wa Mexico na klabu ya Club Tijuana ya Ligi Kuu nchini humo. Wengi wanafananisha uchezaji wake na ule wa Luka Modric.
Mora anashikilia rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kutoa asisti na kufunga bao katika historia ya Ligi Kuu ya Mexico (Liga MX).
Klabu kadhaa kubwa za Ulaya zimeanza kuvutiwa na saini yake, ikiwamo Liverpool, inayojaribu kumsajili kipindi hiki cha kiangazi.
KAREM ALAJBEGOVIC
Winga wa kushoto huyo anakipiga Bayern Leverkusen na alionesha kiwango bora Kombe la Dunia akiwa na kikosi cha timu ya Taifa ya Bosnia.
Alajbegovic (18), ni moja ya makinda wanaomvutia lejendari wa soka wa AC Milan na timu ya taifa ya Sweden, Zlatan Ibrahimovic.
Manchester United ni moja ya klabu kubwa zinazoripotiwa kutolewa macho huduma ya kinda huyo aliyemaliza msimu uliopita akiwa kwa mkopo RB Salzburg.
ALESSANDRO CIRCATI
Beki aliyeng’ara Kombe la Dunia akiwa na timu ya taifa ya Australia iliyofika hatua ya 32 Bora. Circati anakipiga Parma ya Italia.
Katika fainali za Kombe la Dunia zilizomalizika hivi karibuni, Circati alishika nafasi ya pili katika kikosi cha Australia kwa kuwa na idadi nyingi ya pasi sahihi.
Kutokana na uwezo wake, nyota huyo mwenye umri wa miaka 22 anawindwa na klabu ya Brighton ya England.
ALEX FREEMAN
Mlinzi wa Villarreal na alikuwa ‘panga pangua’ katika kikosi cha timu ya taifa ya Marekani msimu huu wa Kombe la Dunia.
Itakumbukwa kuwa beki wa pembeni huyo alikuwa mchezaji muhimu katika kikosi cha kocha Mauricio Pochettino.
Kiwango chake kizuri kimewavutia mabosi wa klabu nyingi kongwe za England, ikiwamo Everton.
MBEKEZELI MBOKAZI
Huyo ni beki wa kati wa timu ya soka ya Taifa ya Afrika Kusini na klabu ya Chicago Fires ya Ligi Kuu nchini Marekani (MLS).
Mbokazi (20), alikuwa kwenye kiwango bora katika mashindano hayo, hasa kwa uwezo wake wa kupiga pasi zinazofika kwa walengwa.
Kwa sasa, huduma yake inazivutia klabu kadhaa, ikiwamo Nottingham Forest, inayotajwa kupeleka ofa yake kwa Chicago Fires.
GUSTAVO PUERTA
Mmoja ya viungo waliofanya vizuri katika fainali hizo. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 22, alikuwa na kikosi cha timu ya Taifa ya Colombia.
Nyota huyo wa Racing Santander, ndiye mchezaji aliyekimbia zaidi katika mchezo ambao Colombia ilipata ushindi dhidi ya Ghana.
Kwa sasa, saini yake ni dili barani Ulaya, ikiwamo Ligi Kuu ya England, ambako anawindwa na Brentford.


