Na mwandishi wetu, Gazetini
LICHA ya changamoto za kidunia, ukiwamo mgogoro wa Mashariki ya Kati unaozihuisha Marekani na Israel dhidi ya Iran, uchumi wa Tanzania umeweza kukua kutoka asilimia 4.7 mwaka 2021 hadi asilimia 5.9 mwaka 2025, huku ukitarajiwa kukua kwa asilimia 6.3 mwaka 2026.
Wakati huo huo, Tanzania imeendelea kuwa kivutio kikubwa kwa wawekezaji kutoka nie, kwa mujibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo.
Prof. Kitila ameyasema hayo Juni 11, 2026, wakati akiwasilisha Bajeti ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa Mwaka wa Mpya wa Fedha wa 2026-27 mjini Dodoma.
Katika hotuba yake, Prof. Kitila amesema ripoti ya hali ya uwekezaji ya Dunia ya UNCTAD ya mwaka 2025 (World Investment Report 2025), inaonesha kuwa uwekezaji kutoka nje nchini ulifikia Dola za Marekani bilioni 1.72 mwaka 2024, ukilinganisha na Dola bilioni 1.34 mwaka 2023.
Huku ukuaji wake huo ukiwa ni wa asilimia 28.3, shughuli za uchimbaji madini na mawe ziliongoza kwa kuwa na uwekezaji mkubwa zaidi wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 442.2.
“Sekta za fedha na bima zilifuata kwa uwekezaji wa Dola za Marekani milioni 401.3, kisha uzalishaji bidhaa viwandani ukiwa wa Dola za Marekani milioni 223.1 na habari na mawasiliano Dola za Marekani milioni 152.1,” amesema Prof. kitila.

Kwa mujibu wa Prof. Kitila, shughuli hizo zilichangia wastani wa asilimia 73.6 ya uwekezaji wote wa moja kwa moja kutoka nje.
Katika hatua nyingine, amesema shughuli za kilimo, ujenzi, na usafirishaji na uhifadhi mizigo zilivutia uwekezaji wa moja kwa moja kwa asilimia 19.4 mwaka 2024, ikilinganishwa na asilimia 5.8 mwaka 2023.
“Kwa ujumla, takwimu zinaonesha kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye ukuaji wa haraka wa uwekezaji barani Afrika (nafasi ya 11 kwa ukubwa wa FDIs),” amesisitiza Prof. Kitila.
Wakati huo huo, ameongeza kuwa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi (TISEZA) ilisajili jumla ya miradi 915 mwaka 2025 yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 10.95, ikilinganishwa na miradi 901 yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 9.3 mwaka 2024.
“Ni sawa na ongezeko la asilimia 17.74 la thamani ya miradi iliyosajiliwa. Idadi hii ya miradi iliyosajiliwa imevunja rekodi ya usajili wa miradi tangu kuanzishwa kwa Kituo cha Uwekezaji (TIC) mwaka 1996 na baadaye TISEZA mwaka 2025.
“Miradi hiyo ipo katika sekta mbalimbali, zikiwemo viwanda, ujenzi wa majengo ya biashara, usafirishaji, utalii na kilimo. Aidha, miradi iliyosajiliwa na TISEZA mwaka 2025 inatarajiwa kuzalisha ajira zaidi ya 162,895,” amesema Prof. Kitila.
HALI YA UCHUMI NCHINI
Prof. Kitila amesema Pato halisi la Taifa lilikua kwa wastani wa asilimia 5.9 na kufikia Trilioni 234.104 mwaka 2025, ikilinganishwa na Trilioni 211.975 (5.6%) mwaka 2024.
“Kutokana na mwenendo huo, wastani wa Pato la Taifa kwa mtu uliongezeka kwa asilimia 7.4 na kufikia shilingi 3,544,124 (dola 1,390) mwaka 2025, ikilinganishwa na shilingi 3,299,637 (dola 1,264) mwaka 2024,” amesema.
Aidha, katika hotuba yake, Prof. Kitila amezitaja sekta zilizokuwa na mchango mkubwa katika Pato la Taifa kuwa ni kilimo kilichochangia asilimia 24.3, ikifuatiwa na ujenzi (11.9%), uchimbaji madini na mawe (10.3%), biashara na matengenezo (8.6%), na usafirishaji na uhifadhi wa mizigo (8.3%).
“Mheshimiwa Spika, sekta zilizoongoza kwa ukuaji ni fedha na bima (15.7%), umeme na gesi (11.8%), uchimbaji wa madini na mawe (9.4%), habari na mawasiliano (8.8%), sanaa na burudani (8.5%), pamoja na usafirishaji na uhifadhi wa mizigo (%8.0),” amesema.
MFUMUKO WA BEI, UMASIKINI UMEPUNGUA
Vilevile, Prof. Kitila amesema mfumuko wa bei kwa mwaka 2025 ulikuwa asilimia 3.3, ikilinganishwa na asilimia 3.1 mwaka 2024, ongezeko hilo likichangiwa na kuongezeka kwa bei za vyakula.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa kiwango hicho cha ongezeko kipo ndani ya lengo la nchi (asilimia 3.0 hadi 5.0), Jumuiya ya Afrika Mashariki (asilimia isiyozidi 8.0) na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (asilimia 3.0 hadi 7.0).
Akizungumzia hali ya umasikini nchini, Prof. Kitila ameeleza kuwa kiwango cha Watanzania wanaoishi katika umasikini wa mahitaji ya msingi kwa Tanzania Bara kimekuwa kikipungua kutoka asilimia 34.4 (mwaka 2007), asilimia 28.2 (mwaka 2012), asilimia 26.4 (mwaka 2018), na asilimia 25.1 (mwaka 2025).
“Mwenendo huu unaonesha kuwa jitihada zaidi zinahitajika katika kuongeza kasi ya kupunguza umaskini ili iendane na kasi ya ukuaji wa uchumi kama ilivyoainishwa katika Dira 2050,” amesema.
MAFANIKIO KUKABILIANA NA UHABA WA AJIRA
Katika hotuba yake, Prof. Kitila amesema kiwango cha ukosefu wa ajira (unemployment) kimepungua na kufikia asilimia 6.2 mwaka 2024, ikilinganishwa na asilimia 8.7 kwa mwaka 2020/21.
Akifafanua zaidi, amesema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Serikali ya awamu ya Sita imeshaajiri watumishi wa umma 32,833, wakiwamo walimu 7,000 na watumishi wa afya 5,000.
Akifafanua zaidi, amesema mbali na malengo mengine, Wizara imejidhamiria kuongeza uzalishaji wa ajira kutoka 981,000 mwaka 2024 na kufikia 1,700,000 mwaka 2026.


