28.3 C
New York

Kwa nini Putin, Trump wanapishana angani kuikimbilia China?

Published:

BEIJING, China

ZIARA ya Vladmir Putin nchini China inakuja zikiwa ni siku chache tu tangu Donald Trump wa Marekani alipomaliza mkutano wake na Rais Xi Jinping mjini Beijing.

Tangu Urusi ilipojitenga na nchi za Magharibi baada ya kuivamia Ukraine, Rais Putin amekuwa karibu zaidi na China, ambapo mataifa hayo yamekuwa washirika wakubwa wa kibiashara na kijeshi pia.

Kwamba Rais Putin amekutana na kufanya mazungumzo mara kadhaa na Xi Jinping tangu Urusi ilipoanza kuishambulia Ukraine (Februari, 2022).

Pia, kumekuwapo na ushirikiano wa kijeshi, kama ambavyo uchunguzi wa Shirika la Utangazaji la Reuters wa mwaka 2025 ulivyofichua kuwa China iliipatia Urusi injini za ndege zisizo na rubani. China ilikana madai hayo.

Rais Trump, ambaye nchi yake ya Marekani ndiyo mshindani mkubwa wa China katika nyanya ya kiuchumi duniani, alikutana na Xi Jinping kwa lengo la kuboresha mahusiano ya kibiashara kati ya mataifa hayo.

Hivyo, kwa mitazamo wa wachambuzi wa siasa za kimataifa, China ndiyo mnufaikaji mkubwa kwa sasa baada ya Marekani na Urusi kuonekana kuikimbilia.

Kwa upande mwingine, ziara ya Putin nchini China imelenga kwenda kuhakikisha mahusiano yao hayaharibiwi na safari ya Trump mjini Beijing.

Ikumbukwe, baada ya nchi za Magharibi kuiwekea vikwazo Urusi, Rais Putin sasa ameifanya China kuwa soko kubwa na muhimu kwa bidhaa zake.

Katika mazungumzo yake na Marekani na Urusi, Rais Xi Jinping anataka kuona migogoro ikifikia ukomo. Vita siyo kipaumbele cha China kwa sasa, na badala yake inataka kuona mazingira rafiki kwa biashara na maendeleo ya teknolojia.

Kwa sasa, Marekani inatibuana na Iran, wakati Urusi iko vitani na Ukraine lakini China inaona migogoro hiyo ikiathiri biashara zake kwa kuwa haitaweza kusafirisha na kusambaza bidhaa katika maeneo hayo.

Mathalan, mgogoro unaoendelea katika Mlango-Bahari wa Hormuz unaotokana na mvutano kati ya Marekani na Iran, umesababisha uharibifu mkubwa wa biashara ya mafuta kwa China, kama ilivyo kwa nchi nyingi duniani.

Wakati huo huo, kutokana na mgogoro unaoendelea Hormuz, Urusi imekuwa muuzaji mkubwa wa mafuta kwa China. Mathalan kwa mwaka 2025, China ilinunua asilimia 18 ya mafuta kutoka kwa marafiki zao hao.

Related articles

Recent articles