Na Mwandishi Wetu, Gazetini-Dodoma
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba, amesema kuwa hadi kufikia Juni 28, 2025 — zikiwa zimebaki siku chache kabla ya kufungwa kwa mwaka wa fedha 2024/25 — sekta ya madini imekusanya maduhuli ya shilingi trilioni 1.063, hivyo kuvuka lengo la awali la trilioni 1.
Akizungumza jijini Dodoma wakati wa kufunga Bonanza la Wizara ya Madini lililoshirikisha watumishi wa wizara na taasisi zake, Mhandisi Samamba alisema kuwa mafanikio hayo yamepatikana licha ya kutokuwepo kwa mgodi mpya katika kipindi husika.
“Hakuna mwaka huko nyuma tuliosogelea hata shilingi bilioni 900, lakini mwaka huu tumeweza kukusanya zaidi ya trilioni moja, sawa na wastani wa bilioni 84 kwa mwezi. Hili ni jambo kubwa kwa taifa,” amesema.

Kwa mwaka wa fedha 2025/26, sekta hiyo imepangiwa kukusanya shilingi trilioni 1.2. Mhandisi Samamba aliwataka watumishi kuongeza bidii, weledi na mshikamano ili kuhakikisha kuwa sekta ya madini inaendelea kuchangia mapato ya ndani na kuiwezesha nchi kujitegemea.
Katika bonanza hilo lililojumuisha michezo mbalimbali kama mpira wa miguu, pete, kuvuta kamba, riadha na kukimbia na magunia, washindi walitunukiwa medali na vikombe. Samamba alisisitiza umuhimu wa mabonanza hayo kama njia ya kujenga mshikamano na afya miongoni mwa watumishi, huku akiagiza yafanyike angalau manne kila mwaka.
Aidha, alitumia nafasi hiyo kupongeza hatua ya Benki Kuu ya Tanzania kuanza kununua dhahabu kama akiba ya taifa, akieleza kuwa hatua hiyo inaipa nguvu sekta ya madini kimkakati.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dk. Janeth Lekashingo, aliwasihi watumishi kuimarisha mawasiliano na mahusiano kazini, huku Katibu Mtendaji wa Tume hiyo, Mhandisi Ramadhan Lwamo, akihimiza umuhimu wa kufanya mazoezi kwa ajili ya afya bora na ufanisi kazini.
Bonanza hilo limeacha ujumbe thabiti wa mshikamano, afya, na mafanikio makubwa katika sekta ya madini kwa mwaka huu wa fedha.


