Na mwandishi wetu, Gazetini
RAIS wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan amesema Afrika inapaswa kuwekeza zaidi katika elimu, ujuzi wa ufundi na uwezo wa kidijitali ili kuwawezesha vijana kuwa wabunifu, wavumbuzi na wazalishaji wa suluhisho, badala ya kubaki watumiaji wa teknolojia zinazobuniwa na wengine.
Akizindua Mkutano Mkuu wa 50 wa Wanahisa na Jukwaa la Miundombinu Afrika leo Jumatano, Agosti 5, 2026 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, Rais Samia amesema rasilimali kubwa zaidi ya Afrika si miundombinu pekee, bali ni watu wake, hususan vijana.
Amesema Tanzania inaendelea kuwekeza katika miundombinu ya kidijitali kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, hatua inayopanua upatikanaji wa huduma za kidijitali, kuboresha huduma za umma, kuimarisha ujumuishaji wa kifedha na kufungua fursa mpya za ubunifu na ujasiriamali kwa vijana.
“Tukiwekeza katika elimu, ujuzi wa ufundi na uwezo wa kidijitali, tutawawezesha vijana wetu kuwa wabunifu na wazalishaji wa suluhisho kwa Afrika na dunia, badala ya kuwa watumiaji wa teknolojia na ubunifu unaotoka kwingine,” amesema Rais Samia.
Ameongeza kuwa pamoja na uwekezaji katika miundombinu, ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi, taasisi za fedha na wawekezaji ni muhimu ili kuharakisha maendeleo ya uchumi na kuifanya Afrika kuwa kitovu cha ubunifu, uzalishaji na ushindani duniani.


