28.6 C
New York

Wajawazito DRC na changamoto ya Ebola

Published:

BUNIA, DRC

MLIPUKO wa ugonjwa wa Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) umeathiri kwa kiasi kikubwa utaratibu wa wajawazito kwenda kliniki, kama anavyoeleza mmoja wao, Esther Lutula.

Esther (26), mama wa watoto wanne na sasa ana ujazito wa miezi minne, anasema ameacha kwenda kliniki kwa ajili ya vipimo vya maendeleo ya ujauzito wake akihofia kukumbana na utaratibu wa kuwekwa karantini.

“Ndiyo maana nasubiri hadi pale ugonjwa utakapokuwa umetulia,” anasema katika mahojiano yake na Shirika la Habari la AP katika Jimbo la Ituri mjini Bunia, ambako ni kitovu cha mlipuko wa Ebola.

Hata hivyo, si Esther pekee. Elodie Yabiri ni mjamzito mwingine aliyeamua kutokwenda hospitali kwa ajili ya huduma ya kliniki, akisema: “Kwa sasa, ukienda hospitali unaambiwa ni Ebola na hapo hapo unawekwa karantini. Ndiyo maana watu wanaogopa.”

Si hao tu. Katika Kliniki ya Benedicte mjini Bunia, idadi ya wajawazito wanaohudhuria imeshuka kutoka 60 hadi 10 kwa mwezi, kwa mujibu wa Dkt. Sonny Mwembo, the medical director.

Hali hii inawapa hofu wataalamu wa afya kwa sababu idadi ya vifo vitokanavyo na uzazi imeongezeka kipindi hiki cha Ebola, hiyo ikitokana na mahudhurio hafifu ya kliniki.

Takwimu zinaeleza kuwa wanawake sita wanafariki kila wiki kutokana na changamoto za wakati wa kujifungua, kwa mujibu wa mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, Noemi Dalmonte.

Lakini, idadi hiyo haihusishi vifo vya nje ya vituo vya afya, ambavyo pia vimetajwa kuongezeka kutoka asilimia 9.1 kabla ya Ebola hadi asilimia 17.4 wakati huu wa mlipuko.

Aidha, tatizo hilo la idadi kubwa ya vifo vya akina mama wajawazito haliko DRC pekee, bali ni changamoto kubwa katika nchi zote za Ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Ni kwa mujibu wa takwimu, ikielezwa kuwa idadi ya vifo vya akina mama wajawazito katika Ukanda huo ni asilimia 70 ya vyote vinavyotokea duniani.

Katika eneo hilo la Kusini mwa Jangwa la Sahara, akina mama wajawazito takribani 180,000 hupoteza maisha kila mwaka, takwimu zinazothibitisha ukubwa wa tatizo.

Related articles

Recent articles