Na Malima Lubasha, Gazetini
WAKAZI wa Kijiji cha Nyambili, Kata ya Sirori Simba, Wilaya ya Butiama mkoani Mara, wameiomba Serikali kujenga zahanati ya kijiji hicho na kuboresha huduma za afya katika Zahanati ya Rwasereta ili kupunguza adha wanazokumbana nazo wanapohitaji matibabu.
Wakizungumza na waandishi wa habari kijijini hapo jana, wananchi hao walisema pamoja na kupongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia huduma ya maji safi na salama, bado wanakabiliwa na changamoto kubwa ya huduma za afya.
Walisema Kijiji cha Nyambili hakina zahanati, hivyo wananchi hulazimika kutembea kati ya kilomita 15 na 18 kufuata huduma katika Zahanati ya Rwasereta au Kituo cha Afya Kiagata, jambo linalowaathiri zaidi wajawazito, watoto na wagonjwa wanaohitaji huduma za dharura.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Majengo, Frank Mwita Wambura, alisema kabla ya mradi wa maji kukamilika wananchi walikuwa wanatumia maji ya visimani yaliyokuwa yakitumiwa pia na mifugo, hali iliyosababisha magonjwa ya tumbo na kuhara kutokana na uchafu wa maji.
Alisema kukamilika kwa mradi wa maji kumepunguza adha hiyo, huku wanawake wakinufaika kwa kupata maji ya bomba karibu na makazi yao badala ya kutembea umbali mrefu kuyatafuta.
“Hata hivyo changamoto kubwa iliyobaki ni ukosefu wa zahanati ya kijiji. Wananchi wanalazimika kwenda Zahanati ya Rwasereta ambayo ipo mbali, jambo linalowaumiza zaidi wajawazito na wagonjwa wanaohitaji huduma za haraka,” alisema Wambura.
Aliongeza kuwa Zahanati ya Rwasereta inakabiliwa na upungufu wa watumishi wa afya, ikiwemo madaktari, wauguzi na wakunga, pamoja na ukosefu wa maabara, mfamasia, vifaa tiba na jengo la wazazi.
Kwa mujibu wake, huduma nyingi za uchunguzi wa magonjwa hazipatikani katika zahanati hiyo, isipokuwa kipimo cha malaria, hali inayowalazimu wagonjwa kwenda vituo vingine kwa ajili ya vipimo zaidi.
Mkazi mwingine, Wilfred Maswi, alisema kabla ya kupatikana kwa maji ya bomba kulikuwa na migogoro ya kifamilia kutokana na wanawake kutumia muda mrefu kutafuta maji, lakini sasa hali hiyo imebadilika.
“Tunamshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea maji safi na salama karibu na makazi yetu. Sasa wanawake hawatumii muda mwingi kutafuta maji kama ilivyokuwa zamani,” alisema.
Kwa upande wao, Bhoke Alfred Mabeche, Rhobi Wambura na Tatu Mtatiro Mahunyo walisema ukosefu wa zahanati katika kijiji chao unawalazimu kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma za afya, huku wakikumbana na changamoto mbalimbali wakati wa kujifungua na kupata matibabu.
Walieleza kuwa katika Zahanati ya Rwasereta kuna chumba kimoja tu cha kulaza wagonjwa wa jinsia zote, jambo linalokosesha faragha na wakati mwingine kuwalazimu baadhi ya wajawazito kulala chini kutokana na uhaba wa vitanda.
“Wakati mwingine wanawake wanaofika kujifungua huwa wengi kuliko uwezo wa vitanda vilivyopo. Wengine hulazimika kulala chini, huku watoto wachanga wakipewa nafasi kwenye vitanda,” walisema.
Waliongeza kuwa chumba hicho hicho hutumika kwa wagonjwa wa kiume na wa kike pamoja na kutoa huduma mbalimbali kama sindano na kujifungua, hali inayopunguza faragha ya wagonjwa.
Wananchi hao wameiomba Serikali kujenga zahanati katika Kijiji cha Nyambili na kuboresha Zahanati ya Rwasereta kwa kuongeza watumishi wa afya, kujenga maabara, jengo la wazazi, kuongeza vitanda na vifaa tiba ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Jitihada za gazeti hili kupata maoni ya Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyambili, Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Rwasereta pamoja na Diwani wa Kata ya Sirori Simba hazikufanikiwa hadi habari hii inaenda kuchapishwa.


