Na mwandishi wetu, Gazetini
VENEZUELA inaendelea kushika nafasi ya kwanza duniani kwa utajiri wa akiba ya rasilimali ya mafuta, licha ya changamoto kubwa za kiuchumi na kisiasa inazokabiliana nazo. Taifa hilo la Amerika ya Kusini linatajwa kumiliki asilimia 17 ya akiba yote ya mafuta duniani, jambo linaloliweka juu ya mataifa yote yanayozalisha au kuhifadhi rasilimali hiyo muhimu.
Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, Venezuela ina akiba ya takribani mapipa bilioni 303 ya mafuta, ambayo bado hayajachimbwa na kuingia rasmi katika soko la dunia. Takwimu hizi zinatokana na ripoti ya hivi karibuni ya Umoja wa Nchi Zinazosafirisha Mafuta Duniani (OPEC).

Ripoti hiyo inaonesha kuwa baada ya Venezuela, Saudi Arabia ndiyo nchi inayofuata kwa utajiri wa akiba ya mafuta, ikiwa na jumla ya mapipa bilioni 267. Mataifa mengine yanayofuata kwa akiba kubwa ni pamoja na Iran, Canada, Iraq, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Kuwait, Urusi na Libya.
Kwa upande wake, Marekani inashika nafasi ya kumi duniani, ikiwa na akiba ya takribani mapipa bilioni 45, licha ya kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa mafuta kwa sasa.
Hata hivyo, tofauti na ukubwa wa akiba yake, Venezuela haifanyi vizuri katika uzalishaji wa mafuta duniani. Nchi hiyo imeachwa mbali na mataifa kama Marekani na Saudi Arabia, ambayo kwa sasa yanaongoza kwa kiwango cha uzalishaji wa kila siku.
Hali hiyo ni tofauti kabisa na ilivyokuwa katika miaka ya 1970, ambapo Venezuela ilikuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa mafuta duniani, ikizalisha hadi mapipa milioni 3.5 kwa siku. Lakini kuanzia miaka ya 2010, uzalishaji wake ulianza kuporomoka kwa kasi.
Kwa mwaka jana, Venezuela iliweza kuzalisha mapipa milioni 1.1 pekee kwa siku, kiwango kinachoonesha kushuka kwa zaidi ya nusu ya uzalishaji wake wa zamani.
Wachambuzi wanataja misukosuko ya kisiasa, usimamizi dhaifu wa sekta ya nishati, pamoja na vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa na Marekani, kuwa sababu kuu zilizoathiri uwekezaji wa kampuni za kigeni na maendeleo ya sekta ya mafuta nchini humo.
Leo hii, licha ya Venezuela kuwa miongoni mwa waanzilishi wa OPEC, ikishirikiana na mataifa kama Iran, Iraq, Kuwait na Saudi Arabia, uzalishaji wake wa kusuasua umeifanya kupoteza ushawishi mkubwa ndani ya umoja huo, licha ya kuwa na utajiri mkubwa wa rasilimali hiyo ardhini.


