9.5 C
New York

TAKUKURU yafichua wizi wa Sh bilioni 147.5 kupitia kadi za benki

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Crispin Chalamila, amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwapo kwa mtandao mpana wa uhalifu wa kifedha unaohusisha kughushi kadi za benki, uliosababisha upotevu wa sh bilioni 147.5 kutoka katika akaunti za wateja bila ridhaa yao.

Chalamila amebaunisha hayo leo, Machi 30, 2026, Ikulu jijini Dar es Salaam, wakati akiwasilisha Taarifa ya Utendaji wa taasisi hiyo mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan.

“Uchunguzi wa awali umebaini kuwepo kwa mtandao wa uhalifu wa kughushi kadi za benki uliosababisha upotevu wa kiasi cha sh bilioni 147.5 kutoka katika akaunti za wateja bila ridhaa yao,” amesema Chalamila.

Ameeleza kuwa fedha hizo zilichotwa kupitia miamala ya malipo ya huduma na bidhaa, ambapo wahalifu walitumia jumla ya kadi 1,551 za wateja kutoka mataifa 11, hali inayoashiria kuwepo kwa mtandao wa uhalifu unaovuka mipaka ya nchi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, miamala hiyo ilifanyika kupitia makampuni 162 kwa kushirikiana na benki tano hapa nchini, ikihusisha sekta mbalimbali zikiwemo utalii, usafirishaji, kodi na bima ya afya.

“Kadi hizi zilihusishwa na miamala iliyofanyika katika mataifa 11, jambo linaloashiria uwepo wa mtandao mpana wa uhalifu wa kifedha unaovuka mipaka ya nchi,” ameongeza.

Aidha, uchunguzi umebaini kuwa makampuni 82 ya utalii katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Dar es Salaam na Mwanza yalihusika katika matumizi ya kadi hizo kinyume cha sheria. Kutokana na vitendo hivyo, baadhi ya benki zilipata hasara ya sh bilioni 2.6 kupitia utakatishaji fedha.

Chalamila amesema hadi kufikia Juni 2025, kiasi cha sh milioni 678 kilikuwa tayari kimeokolewa na kurejeshwa katika taasisi za fedha, huku juhudi za kufuatilia fedha zilizobaki zikiendelea.

“TAKUKURU inaendelea na uchunguzi wa kina ili kubaini wahusika wote na kuchukua hatua stahiki za kisheria dhidi yao,” amesisitiza.

Ubadhirifu NMB wafichuliwa

Katika hatua nyingine, Chalamila ameeleza kuwa TAKUKURU imebaini ubadhirifu wa sh bilioni 19.1 katika Benki ya NMB mkoani Shinyanga, uliotokana na utoaji wa mikopo ya Stakabadhi Ghalani.

Amesema tukio hilo lilihusisha ushirikiano kati ya wakopaji 42, meneja wa dhamana kutoka kampuni ya Brent Intertrade pamoja na baadhi ya watumishi wasio waaminifu wa matawi ya Kahama.

Kwa mujibu wake, kiasi cha sh bilioni 4.2 tayari kimeokolewa na kurejeshwa benki, huku hatua zaidi zikiendelea kuchukuliwa dhidi ya wahusika.

Wakati huo huo, TAKUKURU inaendelea kuchunguza tuhuma za mkataba wenye thamani ya sh bilioni 23 kati ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na kampuni ya Tourist and Hotels Limited unaohusiana na uendeshaji wa Sopa Lodge.

Ripoti ya CAG yafanyiwa kazi

Akizungumzia utekelezaji wa mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2023/24, Chalamila amesema TAKUKURU ilifanyia kazi majalada 86 yenye thamani ya sh bilioni 9.6.

Amesema watuhumiwa katika majalada 13 walichukuliwa hatua za kinidhamu, huku majalada 36 yakiwa yanaendelea kusikilizwa mahakamani.

Aidha, kesi saba zimekwishatolewa uamuzi na Jamhuri ilishinda zote, wakati majalada 30 yalifungwa kutokana na ukosefu wa ushahidi wa kutosha.

Kupitia uchunguzi huo, kiasi cha sh milioni 259.2 kimeokolewa, huku TAKUKURU ikiendelea kufuatilia majalada mengine 169 yanayohusu ubadhirifu wa mapato katika halmashauri mbalimbali nchini.

Taarifa hiyo ya utendaji imewasilishwa sambamba na Taarifa ya Mwaka ya Tathmini ya Utendaji Kazi wa Ununuzi wa Umma na ile ya CAG.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img