Na mwandishi wetu, Gazetini
MAISHA katika miji yote barani Afrika yanatofautiana, hiyo ikitokana na gharama za maisha, ikiwamo uwezo wa watu wake kufanya manunuzi.
Haiishii hapo. Mambo unafuu wa kodi/kujenga nyumba, hali ya usafi, usalama, huduma za afya na hali ya hewa, vinatajwa kuwa vigezo vya ubora wa maisha katika eneo husika.
Sasa, kwa mujibu wa tovuti ya Numbeo, ipo miji ambayo kwa kuzingatia vigezo hivyo, watu wake wanatafsiriwa kuwa wanaishi maisha bora.
Port Elizabeth
Kwa mujibu wa Numbeo, huo ndiyo Mji unaoongoza kwa maisha bora barani Afrika. Port Elizabeth unapatikana nchini Afrika Kusini.
Kuanzia watu wake kumudu gharama za maisha, ikiwamo ujenzi wa nyumba, hadi usafi wa mazingira vinaufanya Mji huo kushika nafasi ya kwanza kwa ubora wa maisha barani Afrika.
Cape Town
Mji mwingine wa Afrika Kusini. Cape Town, licha ya gharama za nyumba kuwa juu, haiuondoshi Mji huo wa Afrika Kusini katika orodha ya maeneo yenye maisha mazuri Afrika.
Ukiweka kando sifa zingine, Cape Town inatajwa kuwa na kiwango kizuri cha usafi wa mazingira, ukilinganisha na miji mingine mikubwa.
Windhoek
Mji Mkuu wa Namibia, ambao pia unasifikia kwa usafi wa mazingira, huku watu wake wakimudu gharama za maisha kwa kiwango kizuri.
Kwa Namibia, gharama za kujenga nyumba nazo ni himilivu kwa wakazi wake wengi, tofauti na ilivyo kwa miji mingine.
Durban
Huo ni Mji mwingine wa Afrika Kusini katika orodha hii. Durban, si tu usafi wa mazingira, bali pia unasifika kwa gharama za kawaida za ujenzi wa nyumba.
Pretoria
Maisha bora mjini humo yanatokana na uwezo mkubwa wa watu wake kumudu gharama za bidhaa muhimu, achilia mbali mfumo mzuri wa upatikanaji wa huduma za kijamii.
Wakati huo huo, hali nzuri ya maisha kwa watu wa mjini Pretoria inatokana pia na gharama nafuu za kujenga nyumba.
Johannesburg
Kigezo cha watu wake wengi kumudu gharama za manunuzi ya bidhaa muhimu kunaufanya Mji huo wa Afrika Kusini nao kutajwa kuwa na maisha mazuri.
Usafi wa mazingizira na gharama himilivu za kumiliki nyumba nazo zinatajwa kuwa ni sifa zingine za Mji huo wa Johannesburg.
Tunis
Licha ya gharama za maisha kuwa za kawaida, Mji huo wa Tunisia hauifanyi vizuri katika usafi wa mazingizira. Hiyo haiondoshi ubora wa maisha yaliyopo Tunis.
Kama ilivyo kwa miji mingine katika orodha hii, gharama za kumiliki nyumba nazo zinatajwa kuwa himilivu kwa wakazi wake.
Casablanca
Mji wa Morocco. Maisha yake ni mazuri lakini haiondoshi ukweli kwamba gharama za kumiliki nyumba ziko juu.
Lakini pia, Casablanca haifanyi vizuri katika usafi wa mazingizira, ukilinganisha na miji mingine iliyotajwa kwenye makala haya.
Nairobi
Mji wa Kenya. Kwa Mji huo, gharama za kumiliki nyumba ziko juu, ingawa wakazi wake wanafurahia ubora wa maisha. Kiwango cha watu wake kufanya manunuzi kiko juu.
Lakini, kama ilivyo kwa Casablanca, Nairobi inakabiliwa na changamoto ya kiwango kikubwa cha uchafuzi wa mazingizira.
Alexandria
Ni Mji mwingine unaotajwa kuwa na maisha bora, licha ya kwamba gharama za bidhaa na huduma ziko juu, ukilinganisha na maeneo mengi barani Afrika.
Si tu gharama za kujenga nyumba ziko juu, bali pia uchafuzi wa mazingizira ni wa kiwango cha juu, tofauti na miji mingine iliyotajwa katika makala haya.


