22.6 C
New York

Wazazi saidieni malezi ya watoto ili kuboresha taaluma

Published:

Na Malima Lubasha, Gazetini– Serengeti

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mapinduzi iliyoko wilayani Serengeti, mkoa wa Mara, Jumanne Nyamhanga, amewataka wazazi na walezi kushirikiana kwa karibu na walimu katika kuwalea watoto wao, hasa nje ya mazingira ya shule, ili kuinua kiwango cha ufaulu ambacho kwa sasa kimeonekana kushuka.

Akizungumza jana katika mkutano wa wazazi ulioitishwa na uongozi wa shule hiyo, Nyamhanga alisema baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakifanya vibaya katika mitihani ya majaribio ya kata na wilaya kutokana na changamoto za malezi wanazokumbana nazo nyumbani, ikiwemo nidhamu duni na matumizi mabaya ya muda.

“Leo ni mara yangu ya kwanza kukutana na ninyi wazazi tangu nimepokea jukumu hili. Lengo la mkutano huu ni kuwapatia taarifa kuhusu maendeleo ya kitaaluma ya watoto wetu, kutatua changamoto zinazowakabili kimaadili, na kujenga ushirikiano wa karibu kati ya walimu na wazazi kwa ajili ya ustawi wa wanafunzi,” alisema Nyamhanga.

Mwalimu huyo alisema kuwa baadhi ya wanafunzi, hasa wa darasa la saba wanaotarajiwa kufanya mtihani wa taifa mwaka huu, wamefanya vibaya katika mitihani ya majaribio, hali inayotia hofu kuhusu maandalizi yao ya mwisho.

Kwa upande wake, Mwalimu wa Taaluma, Mwajuma Ahmed, alisema sababu kuu ya kuitisha mkutano huo ni matokeo mabaya ya mitihani ya mock na ile ya majaribio ya kata, ambayo yanaashiria kuwepo kwa changamoto kubwa katika maandalizi ya wanafunzi.

“Katika mtihani wa mock wa wilaya, kati ya wanafunzi 139 wa darasa la saba, ni wanafunzi 43 pekee waliopata alama A hadi E. Hii ina maana kuwa wanafunzi 96 walishindwa. Hali hii imetushtua sisi walimu na kuona kuna haja ya ushirikiano wa dhati na wazazi kutafuta suluhisho,” alisema Ahmed.

Katika mjadala uliofuata, mzazi Amani Abdallah alisisitiza umuhimu wa wazazi kufuatilia kwa karibu mwenendo wa watoto wao wanapokuwa nyumbani, ikiwa ni pamoja na kuwadhibiti dhidi ya kukesha wakitazama televisheni au kushiriki michezo ya kubahatisha, ambayo inachangia wao kuwa na usingizi wakati wa vipindi darasani.

Naye mzazi Sogita Joseph alitoa wito kwa wazazi kuchangia chakula shuleni ili kuwawezesha wanafunzi kuhudhuria masomo kwa ufanisi, pamoja na kupendekeza utoaji wa majaribio mengi zaidi kwa wanafunzi ili kuwajengea uzoefu wa mitihani.

Aidha, wazazi walikubaliana kuchangia fedha kwa ajili ya kununua rim paper kwa matumizi ya mitihani na majaribio, kutokana na shule hiyo kuwa na mashine ya kudurufu nyaraka.

Mkutano huo ulihitimishwa kwa makubaliano ya pamoja ya kuimarisha ushirikiano kati ya walimu na wazazi katika malezi, nidhamu na maendeleo ya kitaaluma ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Mapinduzi.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img