Na Hassan Mwasha, Gazetini
HIVI karibuni, rapa wa Marekani, Nicki Minaj, alitoa kauli tata kuhusu soko la muziki, akisema limejaa vishawishi vinavyoweza kukutoa kwenye imani ya dini. Kwa ufupi, kuna ushetani mwingi.
Minaj aliongeza kuwa wapo watu kwenye soko la muziki, ambao wamekuwa ‘miungu-watu’ wa kutesa wasanii, ikiwamo kuwalazimisha kufanya mambo mabaya ili kuwapa sapoti ya kuendelea kusikika.
Ni kauli nzito, hasa inapotoka kwa msanii wa daraja la juu kama Minaj. Kama staa wa hadhi yake anapitia misukosuko ya aina hiyo, vipi kwa wasanii wachanga kwenye gemu? Inafikirisha.
Kwa upande mwingine, kauli ya Minaj inaweza kuturudisha hapa nyumbani. Soko la muziki wa kizazi kipya (Bongo Fleva). Kivipi?
KAULI YA VANESSA MDEE
Desemba 16, 2024, bibiye huyo aliyewahi kufanya vizuri Bongo Fleva, alitoa maoni yanayoendana na alichokisema Minaj, kwamba muziki umejaa ushetani.
“Sekta ya muziki ni ya kitamaduni sana. Watu wanatumia miungu sana (watu wanategemea sana miungu),” alisema Vanessa, ambaye ameokoka na kuachana kabisa na Bongo Fleva.
Aidha, Mdee aliyewahi kutamba na ‘Cash Madam’ na ‘Nobody But Me’, alifichua alivyowahi kushawishiwa kwenda kwa mtaalamu (mganga) kabla ya kupeleka wimbo sokoni.
“Sekta ya muziki sio ya kupendeza kama inavyoonekana. Nyuma ya matukio, kuna giza jingi—mila za kishetani, mazoea yenye kutiliwa shaka, na kujipoteza mwenyewe,” alisema.
BILLNASS AFUNGUKA, AONYA VIJANA
Miezi sita baadaye, aliibuka rapa anayefanya vizuri Bongo Fleva, Billnass, kupitia Instagram akiwa na mtazamo huo huo, kwamba tasnia ya burudani imejaa mambo mengi mabaya.
Ilikuwa Juni 11, 2025, ambapo alisema umaarufu katika sanaa ni chanzo cha vita,usaliti,ushetani na dhuluma. Aliandika:
“… Kabla ya kuingia kwenye tasnia yoyote inayohusiana na umaarufu Tanzania, muombe sana Mungu akupe nguvu ya uvumilivu na roho ya kustahimili.
“Huku kuna kila aina ya vita, usaliti, ushetani, dhuluma kuanzia kwa wadau, ‘managers’ (mameneja), ‘distribution company’ (kampuni za usambazaji) na ‘labels’ (lebo).”
Kuhusu picha waliyonayo wasanii chipukizi juu ya maisha mazuri yaliyopo kwenye soko la muziki, Billnass alisema siyo rahisi kama inavyodhaniwa na vijana wengi.
Kwake, kutajirika kupitia sanaa, ikiwamo muziki, ni ngumu kuliko kupata msongo wa mawazo, maradhi, kuingia kwenye vilevi, na hata kupoteza maisha.
“Ni vyema kuwa makini sana na kuingia kwenye tasnia ukiwa na utayari lakini usiache kumuweka Mungu kwanza.
“Maana unaweza kupambana ili uisaidie familia yako, kumbe unaenda kuleta janga ambalo familia yako itakuwa kwenye jukumu la kuteseka kukusaidia,” alionya Billnass.
Kwa upande wake, mkongwe wa Bongo Fleva, Godfrey Tumaini ‘Dudu Baya’, amekuwa akisisitiza hilo mara kadhaa, kwamba kiwanda hicho, pamoja na tasnia ya burudani kwa ujumla, vimejaa ushetani, vikiwamo vitendo vya mapenzi ya jinsia moja.
MIFANO HAI
Licha ya mafanikio yake makubwa katika kuzalisha ajira nyingi kwa vijana, bado Bongo Fleva ina doa la mastaa wake kuingia kwenye matumizi ya dawa za kulevya au ulevi wa pombe uliopindukia.
Kwa nyakati tofauti, wasanii Chid Benz, Lord Eyez, Daz Baba, Ferouz, Young D na Jose Mtambo, kwa kuwataja kwa uchache, waliingia kwenye shimo hilo.
Hata hivyo, bado kumekuwapo na hisia mseto (maoni tofauti) katika jamii juu ya nadharia ya ustaa wa muziki au sanaa kwa ujumla kuhusishwa na matukio ya aina hiyo (ushetani).
Kwamba wapo wanaoamini ni kweli, kwamba tasnia ya burudani ina ‘mawakala wa shetani’, ambao wamekuwa wakitumia nafasi na pesa zao kushawishi wasanii kufanya mambo yasiyofaa kama sharti la kuwasaidia kubaki kwenye ramani.
Pia, wapo wanaokinzana na mtazamo huo, wakiamini wasanii hujiingiza wenyewe katika tabia zisizofaa kwenye jamii kutokana na kulewa sifa na mafanikio.


