23.4 C
New York

UDOM yang’ara Nanenane kwa ubunifu, teknolojia

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

CHUO Kikuu cha Dodoma (UDOM) kimeendelea kuthibitisha nafasi yake kama kitovu cha utafiti, ubunifu na teknolojia nchini baada ya kuwasilisha bunifu mbalimbali zinazolenga kutatua changamoto za jamii katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma.

Akizungumza jana, Agosti 7, 2026, baada ya kutembelea banda la UDOM, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Jabiri Omari Makame, amesema ameridhishwa na kiwango cha ubunifu kinachoendelea chuoni hapo, akibainisha kuwa tafiti zinazofanywa zina mchango mkubwa katika sekta za kilimo, afya, teknolojia na maendeleo ya taifa.

Amesema miongoni mwa bunifu zilizomvutia ni teknolojia ya kisasa inayoweza kutambua kiwango cha unyevunyevu wa udongo na kuwasha mfumo wa umwagiliaji moja kwa moja bila kuhitaji usimamizi wa binadamu.

Kwa mujibu wa Makame, teknolojia hiyo inaweza kusaidia kuongeza tija katika kilimo kwa kuwawezesha wakulima kutumia maji kwa ufanisi zaidi.

“Nimefurahishwa pia na ubunifu wa vifaa vya kisasa vinavyoweza kurekodi taarifa muhimu za gari wakati wa ajali, ikiwemo mwendo na mazingira ya tukio. Teknolojia hii ni kama ‘black box’ ya ndege, lakini kwa magari ni ‘white box’,” amesema.

Katika sekta ya afya, Makame amesema UDOM imeonyesha maendeleo makubwa kupitia tafiti za dawa mbalimbali, zikiwemo zinazolenga kutibu vidonda vya tumbo pamoja na mafuta ya tiba yaliyotengenezwa kwa kutumia malighafi asilia bila kemikali hatarishi.

Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Fedha, Mipango na Utawala wa UDOM, Profesa Jeifta Sunzu, amesema ushiriki wa chuo hicho katika Maonesho ya Nanenane unalenga kuonyesha kazi za utafiti, ubunifu na teknolojia zinazofanywa na chuo kwa manufaa ya Watanzania.

Amesema UDOM tayari imeandaa mitaala mipya inayohusu Akili Unde (Artificial Intelligence), ambayo imewasilishwa na kuidhinishwa na mamlaka husika.

Profesa Sunzu amewahimiza wazazi na walezi kuwapeleka watoto wao UDOM ili wapate elimu na maarifa yanayoendana na maendeleo ya sayansi na teknolojia duniani.

Related articles

Recent articles