Rais wa Simba SC, Mohammed Dewji, amewataka wanachama na mashabiki wa klabu hiyo kutogawanyika, akisisitiza kuwa Simba ni kubwa kuliko changamoto yoyote inayokabili klabu hiyo na kwamba mabadiliko yaliyopitishwa na wanachama yanapaswa kukamilishwa.
Dewji ameyasema hayo leo wakati wa Tamasha la Simba Day lililofanyika katika kusherehekea miaka 90 ya klabu hiyo.
Akizungumza mbele ya mashabiki, Dewji amesema mabadiliko ya klabu hiyo yalianza miaka kadhaa iliyopita na yalipata ridhaa ya wanachama, lakini hadi sasa hayajakamilika.
Amesema bajeti ya takribani Sh bilioni 30 iliwekwa kwa ajili ya mchakato huo, huku akijiuliza sababu za mabadiliko hayo kuchelewa kukamilika licha ya kuwa wanachama wenyewe walishayapitisha.
“Mpaka leo mabadiliko tuliyoanza hayajakamilika. Mpaka lini? Kama ninyi wenyewe mliridhia mabadiliko haya, kwa nini baada ya miaka 10 bado tunakwama?” alihoji Dewji.
Aidha, alihoji iwapo ni sahihi watu wachache kuzuia matakwa ya wanachama wengi wanaotaka kuona klabu hiyo ikifanya mabadiliko na kusonga mbele.
Dewji pia amesema kumekuwa na taarifa mbalimbali zinazotolewa kumhusu ambazo si sahihi, lakini amechagua kukaa kimya kwa kuwa anaamini maslahi ya Simba ni makubwa kuliko yeye binafsi.
“Mengi yanasemwa juu yangu ambayo si sahihi, lakini nimechagua kukaa kimya kwa sababu maslahi ya Simba ni makubwa kuliko mimi,” amesema.
Kuhusu suala la kadi za wanachama, Dewji amesema mchakato huo hauzuiwi na yeye wala upande wa mwekezaji, akisisitiza kuwa lengo lake ni kuona Simba inajengwa kwa manufaa ya klabu na wanachama wake.
“Lengo langu ni kujenga Simba na siyo kufaidisha watu wachache. Ndiyo maana nawaomba sana Wanasimba wenzangu, mnapoambiwa jambo, hojini, ulizeni na tafuteni ukweli,” amesema.
Dewji aliwataka wanachama na mashabiki kuepuka kugawanyika na badala yake kuungana katika kukamilisha mabadiliko yanayolenga kuipeleka klabu mbele.
“Jambo la muhimu tusigawanyike. Simba haiwezi kujengwa kama taa, kuwashwa na kuzimwa. Badala yake tukamilishe mabadiliko na twende mbele. Mimi niko tayari kufanya sehemu yangu, lakini Simba siyo ya MO pekee. Safari tuliyoanza lazima tuikamilishe,” amesema.
Alisisitiza kuwa Simba ni mali ya Wanasimba wote na kwamba changamoto zinazokabili klabu hiyo hazipaswi kuwa sababu ya wanachama kugawanyika.
“Simba ni kubwa kuliko changamoto yoyote tunayopitia leo. Tusikubali kugawanyika. Simba ni yetu, twende mbele,” amesema Dewji.


