Na mwandishi wetu, Gazetini
JORGE Messi, baba na wakala wa muda mrefu wa nyota wa Argentina na Inter Miami, Lionel Messi, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 68.
Jorge alifariki Ijumaa katika hospitali iliyopo Rosario, Argentina, baada ya kuugua kwa muda mrefu. Taarifa za kifo chake zimethibitishwa leo Jumamosi. (ESPN)
Familia ya Messi ilikuwa imeweka hali ya afya ya Jorge kuwa suala la faragha, kabla ya kutoa taarifa wakati wa Kombe la Dunia mwaka huu kwamba alikuwa akipitia changamoto za kiafya na kupata matibabu chini ya uangalizi wa madaktari.
Baada ya kufunga bao katika mchezo wa kwanza wa Argentina dhidi ya Algeria katika Kombe la Dunia mwezi Juni, Lionel Messi alionekana kuwa na hisia kali, akisema hisia hizo “hazikuwa na uhusiano na soka.”
“Nimepitia siku ngumu na zenye changamoto. Ninashukuru kwa msaada niliopewa na wachezaji wenzangu pamoja na benchi la ufundi katika kipindi hiki,” amesema Messi.
Wiki moja baadaye, familia ya Messi ilitoa taarifa ikisema Jorge alikuwa akipitia changamoto ya kiafya, lakini hali yake ilikuwa ikiendelea vizuri chini ya uangalizi wa madaktari.
Jorge Messi alikuwa mtu muhimu katika safari ya soka ya mwanaye. Alikuwa wakala wake na mshauri wake wa karibu tangu miaka ya mwanzo ya taaluma yake, akihusika katika maamuzi muhimu yaliyomsaidia Lionel Messi kujenga moja ya taaluma zilizofanikiwa zaidi katika historia ya soka.
Jorge alitokea Rosario na awali alifanya kazi katika kiwanda cha chuma kabla ya familia hiyo kuhamia Ulaya mwaka 2000, wakati Lionel Messi alipojiunga na akademi ya Barcelona.
Baadaye aliendelea kusimamia masuala ya taaluma ya mwanaye, katika kipindi ambacho Messi alicheza Barcelona, Paris Saint-Germain na hatimaye kujiunga na Inter Miami.
Katika kipindi hicho, Messi aliweka rekodi mbalimbali akiwa Barcelona, ikiwemo kuwa mchezaji aliyecheza mechi nyingi zaidi na kufunga mabao mengi zaidi katika historia ya klabu hiyo. Pia ameshinda tuzo ya Ballon d’Or mara nane, rekodi ya mchezaji mmoja.
Kwa upande wa timu ya taifa, Messi aliisaidia Argentina kufika fainali tatu kati ya nne za Kombe la Dunia zilizopita, ikiwemo kutwaa ubingwa mwaka 2022 nchini Qatar.
Kufuatia kifo cha Jorge, klabu ya Newell’s Old Boys, ambayo ni klabu ya kwanza ya Lionel Messi, ilikuwa miongoni mwa taasisi za kwanza kutoa salamu za rambirambi.
“Newell’s Old Boys inaomboleza kwa maumivu makubwa kifo cha Jorge Messi,” klabu hiyo ilisema katika taarifa.
Klabu hiyo ilimtaja Jorge kama shabiki mkubwa wa Newell’s Old Boys na mtu ambaye alikuwa nguzo muhimu katika safari ya Lionel Messi, akishirikiana na mke wake, Celia, kumsaidia mwanaye katika hatua mbalimbali za maisha na taaluma yake.
Jorge ameacha mke wake, Celia, na watoto wake wanne; Lionel, Rodrigo, Matías na María Sol.
Lionel Messi alikuwa pamoja na familia yake huko Rosario baada ya kumalizika kwa Kombe la Dunia kabla ya kurejea Marekani kuendelea na majukumu yake katika klabu ya Inter Miami. (Reuters).



