Na Benjamin Madaha
KATIKA kipindi hiki cha tatizo la ajira, watu wanatafuta pesa kila kukicha -wengine usiku na mchana na wengine hujaribu kuhama eneo moja kwenda eneo jingine kutafuta pesa.
Wengine wamekuwa ombaomba, wengine wanalalamikia Serikali kubana hela na uchumi, wengine wamekata tamaa na kujitamkia kuwa wao wamezaliwa masikini waliorithi na watakufa hivyo.
Katika Makala ya leo, nitabadilisha kabisa mawazo yako na kuanza ukurasa mpya.
Ukweli ni kwamba huwezi kutafuta kitu wakati hujui hata kilipo. Huwezi kutafuta maji angani wakati yapo mtoni, ziwani nk.
Huwezi kutafuta ‘cement’ katika majivu. Ukitaka mbolea, nenda katika zizi. Huwezi kupata maembe katika mti wa chungwa n.k. Kila kitu kinapatikana mahala pake.
Swali; pesa zimejificha wapi? Wengine wanasema pesa ni adimu sana kuzipata lakini nikwambie hivi; pesa ziko karibu sana na wewe kuliko unavyoweza kufikiria.
Je, unatafuta pesa? Je, umechoka na maisha yako ya kipato cha chini? Soma maeneo au sehemu hizi 10 ambazo pesa zimejificha. (Hakikisha una kalamu na daftari).
Katika utafiti wangu binafsi juu ya pesa, niligundua ukweli huu ambao unasema “watu wengi huangalia, lakini ni watu wachache wanaona.”

Kwa miaka, nimesikia watu wakilalamika kutokuwa na pesa na kutoweza kupata pesa za kufanya kile wanachotaka kufanya. Kisha mtu atataka kuuliza swali hili ‘PESA ZIMEJIFICHA WAPI?’
Nimegundua sehemu 10 ambapo pesa zimefichwa na tunapochunguza moja kwa moja, nataka uwe nyeti sana na utafakari kwa sababu nimeona watu wengi wakiwa huru kifedha kwa ugunduzi na utafiti huu tu.
Pesa zimejificha kwa watu
Popote watu walipokusanyika, pesa pia ipo. Kama una ‘account’ mtandaoni na kuna ‘followers’, basi hapo kuna pesa. Pesa zote ambazo umewahi kuhitaji ziko mikononi mwa watu. Pesa hazianguki kutoka mbinguni.
Suala ni nini ufanye ili kutoa pesa zao mfukoni wakupe? Kawaida, watu hawawezi kukupa pesa kwa sababu tu unataka. Walakini, wakati utakapowapa kitu ambacho wanathamini, watakupa pesa zao kwa furaha.
Pesa zimejificha katika matatizo
Pesa zimejificha katika shida.Kila shida unayoiona, ni pesa iliyojificha. Badala ya kulalamika juu ya shida, kila msomaji anapaswa kuanza kufikiria suluhisho kwa sababu kuona shida na kuitatua ndio huleta pesa.
Angalia katika mazingira ya karibu na wewe, kila shida unayoona, kila hitaji unaloliona karibu ni uwezekano na fursa ya kukuingizia pesa. Shida ya mtu mmoja ni fursa ya mtu mwingine.
Muuzaji wa chakula huingiza pesa kutokana na shida yako ya njaa. Muuzaji wa nguo hupata pesa kutokana na shida yako ya uchi/mtindo.
Daktari huingiza pesa kutokana na shida yako ya kiafya. Wakili hufanya pesa kutokana na shida yako ya Kesi. Mwalimu hupata pesa kulingana na shida yako ya ujinga.
Pesa zimejificha katika talanta/vipaji
Hakuna mtu hata mmoja duniani ambaye hana kipawa au talanta katika eneo moja. Muumbaji alihakikisha kuwa hakuna mtu aliyeumbwa tupu.
Wewe unayesema huna kipaji, usirudie tena kusema hivyo. Kama wanadamu, tumejazwa na uwezo wa ndani Ili kutusaidia katika safari ya maisha.
Kuna watu wengi mashuhuri, ikiwa sio kwa talanta na zawadi zao, wasingeweza kupanda ngazi ya ukuu na umaarufu. Mfano; Mbwana Samatta, Diamond Platinumz, Lionel Messi n.k.
Pesa zimejificha katika fursa
Sababu ambayo watu wengi leo ni masikini ni kwamba wanazipita fursa mara kwa mara. Kwa Kingereza, umasikini tunaita ‘P.O.O.R’ (Passing Over Opportunities Repeatedly).
Wengi wanaziona fursa lakini wanaogopa kuchukua hatua wakihofia watapoteza au kutapeliwa, bila kujua kwamba hizi ni kama dhahabu isiyosafishwa ambayo inaweza kubadilisha maisha yao milele.
Pesa zimejificha katika bidhaa/huduma
Fikiria kwa muda. Umetumia kiasi gani katika miezi 12 iliyopita? Ulitumia pesa kwenye nini? Jibu liko wazi kabisa.
Umetumia 80% ikiwa sio 100% kulipia bidhaa na huduma. Hii inamaanisha kwamba pesa imetoka kwako kwenda kwa wengine kwa bidhaa na huduma.
Haishangazi kwa nini sarafu hutumiwa kuelezea ‘pesa’ kwa sababu, ni kama mikondo ambayo inapita kuelekea kwako au mbali na wewe.
Pesa imejificha katika bidhaa na huduma na wale ambao wana bidhaa au wanatoa huduma wanaendelea kupata pesa wakati wote, iwe kuna uchumi au hakuna uchumi.
Pesa zimejificha katika wazo
Vitu vyote unavyoviona duniani sasa hivi ni wazo la mtu lililofanyiwa kazi. Kuna watu walipoona miti wakaja na wazo la kutengeneza meza, viti, vitanda, n.k.
Mark Zuckerberg, mgunduzi wa Facebook, alipata wazo na kulifanyia kazi na leo hii unaona FB.
Pesa zimejificha katika maono
Ndiyo, katika maono ya watu kuna pesa. Wengine wanasema pesa ni adimu lakini nakwambia pesa ziko karibu sana na wewe kuliko unaweza kufikiria.
Kwa Wakiristo, Biblia inasema bila maono watu wanaangamia. Maono ni jicho ambalo hukuruhusu kusonga mbele maishani. Mtu asiye na maono ni kama gari linaloendeshwa usiku bila taa.
Makampuni na mashirika mengi yanayostawi leo yanajengwa kupitia maono kutoka kwa waanzilishi. Pata maono, shiriki maono, na uyafanyie kazi, na maono hayo yatabadilishwa kuwa pesa.
Pesa zimejificha katika ujuzi/maarifa
Ujuzi ni uwezo wa kufanya kazi fulani vizuri. Maarifa ni uelewa wa jambo fulani vizuri. Dunia hii inatoa fursa kubwa kwa watu wenye ujuzi na maarifa na pesa zinapatikana vizuri tu.
Pesa zimejificha katika mbegu
Mbegu ni mtaji. Unaweza kujitolea leo kwa ajili ya kesho bora.( Mbegu ni mtaji) Mbegu yako inaweza kuwa muda wako, kuchelewa kulala na hata pesa.
Pia, inaweza kuwa nguvu, maumivu, uvumilivu, kujitolea, kujinyima au kitu chochote unachoweza kutumia kama aina ya mtaji ambayo inaweza kutoa kipato usichoweza kufikiria.
Pesa zimejificha kwa Mungu
Nani ameunda iPhone? Jibu rahisi ni Steve Jobs au kampuni yake Apple. Watu wanaangalia kitengo cha bidhaa cha Apple na wanashangazwa na fikra ambayo Steve Jobs alizipata. (Natumia mifano ya watu maarufu lakini usiione kuwa makala hii haikuhusu).
Je, unamtazamaje mwanadamu, kiumbe tata na mifumo mingi inayofanya kazi mara moja, na unafikiria tulianguka tu kutoka angani? Hapana.
Tunaye Muumba, hiyo ni hakika. Mungu ndiye alimuumba mwanadamu. Je, kuna jambo gani gumu sana kwa Mungu kufanya? La hasha! Aliumba Mbingu na Dunia. Anahifadhi dunia na mbingu kwa kusimamishwa bila nguzo au yeyote.
Mwalimu Benjamin Madaha ni mchambuzi mbobezi wa masuala ya fedha.


