25.4 C
New York

Missy Elliott: Safari ya ustaa na baba alivyotaka kumpiga risasi

Published:

LOS ANGELES, Marekani

JINA lake ni Melissa Arnette lakini wapenzi wa muziki wa R&B na Hip hop, hasa katika miaka ya 1990, wanamfahamu kwa jina la ‘Missy Elliott’, na wengine wachache wakimwita ‘Misdemeanor’.

Kwa ufupi, ni lejendari mwenye tuzo nne za Grammy. Mmoja ya marapa wenye mauzo makubwa kwenye kazi zao kwenye historia ya Hip hop.

Kama hiyo haitoshi, anayezungumziwa hapa ni mwanamuziki ambaye mwaka 2020 alitajwa na Billboard kushika naafsi ya tano katika orodha ya wasanii 100 wenye video kali.

Mwaka 2021, kama itakumbukwa, Missy Elliott alikuwa rapa wa kike wa kwanza mwenye ngozi nyeusi kutambuliwa na Rock and Roll Hall of Fame.

ALIANZIA KANISANI

Alizaliwa Julai Mosi, 1971 huko Virginia, akiwa mtoto pekee wa bi. Patricia na Ronnie Elliott. Licha ya ugumu wa maisha kwenye familia, Missy Elliott alipenda kwenda kanisani, ambako alianza kuimba kwaya akiwa na umri wa miaka minne tu.

“Mbali ya umasikini, shida nyingine kubwa iliyokuwepo nyumbani ni baba kumtesa mama, ikiwamo kumvunja bega wakati fulani,” anasimulia Missy Elliott.

Mkongwe huyo anakumbuka pia tukio la kutisha la baba yake kumtolea bastola wakati akijaribu kumtetea ‘bi mkubwa’.

“Mama aliamua tuondoke na kwenda kuishi kwa ndugu yetu mjini Portsmouth na huko ndiko nilikomaliza elimu ya sekondari,” anasema Missy Elliott.

Kwa sasa, anakiri kuwa amekuwa akiwasiliana kwa simu na mzee wake huyo lakini hawezi kusahau na kumsamehe kwa namna alivyowapitisha kwenye mateso.

SAFARI YA MUZIKI, MAFANIKIO

Ilianzia mwaka 1988 baada ya Missy Elliott na mabinti wenzake watatu – La’Shawn Shellman, Chonita Coleman na Radiah Scott – kuanzisha Kundi la muziki wa R&B la Fayze, ambalo baadaye lilifahamika kwa jina la Sista.

Ngoma ya kwanza ya Kundi iitwayo ‘Brand New’ ilitoka mwaka 1993 lakini mafanikio makubwa ya Missy Elliott yalikuja baada ya kuachia albamu yake mwenyewe ya ‘Supa Dupa Fly’ mwaka 1997.

Supa Dupa Fly ni albamu iliyoleta mapinduzi makubwa katika soko la muziki wa R&B/Hip hop, ikishika nafasi ya tatu katika chati za Billboard 200.

Iliweza hata kuingia kwenye kinyang’anyiro cha Albamu Bora ya Mwaka ya Hip hop katika tuzo za Grammy lakini ilizidiwa kete na ‘No Way Out’ ya mkali P. Diddy.

Wakati huo, Missy Elliott alishajiingiza kwenye utayarishaji wa muziki akishirikiana na prodyuza aitwaye Timbaland, ambapo walihusika katika ngoma tisa za albamu ya ‘One in a Million’ ya staa wa wakati huo, Aaliyah (sasa marehemu).

Pia, mbali ya kuandika baadhi ya ngoma, pia Missy Elliott alishiriki kutayarisha (kama prodyuza) albamu ya mkali Whitney Houston ya ‘My Love Is Your Love’ iliyoingia sokoni mwaka 1998.

Albamu yake ya pili, ‘Da Real World’ ya mwaka 1999, ilikuwa na ngoma ya ‘Hot Boyz’, ambayo iliweza kukaa namba moja kwa wiki 18 kwenye chati za Hot Rap Songs. Iliuza nakala milioni 1.5 kwa Marekani na milioni tatu duniani kote.

Kilele cha mafanikio kilifuata katika albamu ya tatu (Miss E … So Addictive, 2001) na ya nne (Under Construction, 2002), ambazo zilimpa tuzo ya Grammy.

Hiyo ya ‘Miss E … So Addictive’ ilishika nafasi ya pili katika chati za muziki Uingereza, pia ikiuza nakala 250,000 ndani ya wiki moja tu tangu iingie sokoni.

Hata albamu yake ya tano, This Is Not a Test (2003) na ‘The Cookbook’ (2005) nazo zilikuwa na mafanikio makubwa, ikiwamo wimbo wa ‘Lose Control’ kufanya vizuri katika chati za Billboard.

Related articles

Recent articles