25.4 C
New York

Mjadala wa nani mkali kati ya Tupac, Eminem unavyokosa majibu

Published:

DETROIT, Marekani

NI miaka zaidi ya 30 tangu Tupac Shakur alipofariki. Ni miaka zaidi ya hiyo tangu Eminem alipoanza kuwika katika soko la muziki wa Hip hop nchini Marekani.

Kwa miaka mingi, umekuwapo mjadala mzito katika tasnia ya muziki huo, ukihusisha mashabiki wa wasanii hao. Mjadala wa nani mkali kati ya Tupac na Eminem.

Isivyo bahati, ni mjadala uliokosa majibu ya kumaliza utata, hivyo kila upande ukibaki na msimamo wa kuamini msanii wake ndiye mkali.

Wakati Eminem akipendwa zaidi na vijana, Tupac ana ushawishi mkubwa kwa watu wazima wanaotaja nyimbo zake kuchagiza harakati za kumkomboa mtu mweusi nchini Marekani, kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa kwa nyakati tofauti na majukwaa ya kidigitali ya Reddit, X na YouTube.

Kwanini hakuna mshindi kila unapoibuliwa mjadala wa nani mkali kati ya Tupac na Eminem? Ni kwa sababu marapa hao wana sifa zinazowatofautisha na kumfanya kila mmoja awe bora kuliko mwenzake.

Mathalan, kwa ufundi wa kucheza na maneno, na kasi ya ‘kuchana’ na kubadilisha miondoko katikati ya ‘verse’, Eminem ni habari nyingine. Anatajwa kuwa ni mmoja ya marapa bora wachache wenye uwezo mkubwa katika eneo hilo.

Unaweza kujiridhisha kwa kusikiliza ‘Rap God’, ‘Technical Difficulties’ na baadhi ya zilizomo kwenye Album yake maarufu ya ‘The Eminem Show’.

Tupac hakuwa na uwezo huo. Na badala yake, alimzidi mno Eminem linapokuja suala la masimulizi (storytelling) na kuandika vitu vinavyogusa hisia, kama alivyofanya katika nyimbo ‘Dear Mama’, ‘Changes’ na ‘California Love’.

Kwa maana nyingine, Tupac aliweza kuyachukua maisha ya mtaani na kuyawasilisha kupitia ngoma zake, hivyo kuwavutia si tu mashabiki, bali hata wasanii chipukizi. Kwa ufupi, ndiye ‘role model’ wa Kendrick Lamar, J. Cole na wengine kibao.

“Eminem ni fundi. Tupac alikuwa mshairi wa kimapinduzi. Walitofautiana hapo na ndiyo maana mjadala huo hautakwisha,” alisema mwandishi wa habari za Hip hop,  Soren Baker.

Katika eneo la biashara, Eminem ni zaidi ya Tupac. Nyimbo kama ‘Lose Yourself’, ‘Stan’ na ‘Till I Collapse’ zilimpa mabilioni ya fedha, hivyo ni rapa aliyefanikiwa zaidi sokoni kuliko Tupac.

Lakini, wakosoaji wanasema ni ngumu kumfananisha na Tupac, ambaye aliondoka duniani akiwa na umri mdogo wa miaka 25 tu baada ya kupigiwa risasi mwaka 1996 mjini Los Angeles.

Kama hiyo haitoshi, wakosoaji wanaona Tupac angeweza kupata fedha nyingi zaidi ya alizoingiza endapo angekuwa rapa wa kizungu, kama ilivyo kwa Eminem.

Msingi wa hoja hiyo unatokana na ukweli kwamba Tupac aliishi katika zama ambazo kila kona ya mtaa nchini Marekani ilikuwa na harufu ya vitendo vya ubaguzi wa rangi dhidi ya watu weusi.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img