10.9 C
New York

Wananchi 1,700 kulipwa bilioni 5.1 kupisha mradi wa umeme Mtwara-Lindi

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limezindua rasmi zoezi la ulipaji fidia kwa wananchi wanaopisha utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 220 kutoka Masasi mkoani Mtwara hadi Mahumbika mkoani Lindi.

Akizungumza Mei 7, 2026 katika Kata ya Kiwalala, Halmashauri ya Mtama, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange, amesema Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika miradi ya umeme ili kuhakikisha mikoa ya kusini inaunganishwa kwenye Gridi ya Taifa.

Twange amesema zaidi ya Sh bilioni 5.1 zimetengwa kwa ajili ya kuwalipa fidia wananchi takribani 1,730 katika mikoa ya Lindi na Mtwara watakaopisha mradi huo mkubwa wa miundombinu ya umeme.

Amefafanua kuwa katika awamu ya kwanza, kaya 78 kutoka vijiji vya Kiwalala na Mahumbika zitanufaika na zaidi ya Sh milioni 253 kabla ya zoezi hilo kuendelea katika vijiji vingine vilivyopo kwenye mradi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Victoria Mwanziva, amesema ulipaji wa fidia unalenga kuhakikisha wananchi wote wanaopitiwa na mradi huo wanapata stahiki zao kwa wakati ili kurahisisha utekelezaji wa mradi huo wa maendeleo.

“Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuidhinisha zaidi ya Sh bilioni 5.1 zitakazotumika kuwalipa fidia wananchi zaidi ya 1,700 katika maeneo ya Lindi na Mtwara,” amesema Mwanziva.

Zoezi hilo litafanyika katika vijiji 46 vya wilaya za Lindi, Ruangwa, Newala na Masasi, huku likianza na vijiji 14 vya Halmashauri ya Mtama.

Mradi huo unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika katika ukanda wa kusini mwa Tanzania na kupunguza utegemezi wa mfumo wa sasa wa usafirishaji wa umeme kutoka vituo vya gesi asilia vya Mtwara.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img