Na mwandishi Wetu, Gazetini
SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kuchukua hatua madhubuti katika kuimarisha sekta ya madini kama nguzo muhimu ya ukuaji wa uchumi wa Taifa, ikiwa ni utekelezaji wa Madini Vision 2030. Hatua hiyo inajidhihirisha kupitia uanzishwaji wa mradi mkubwa wa ujenzi wa Kituo cha Kisasa na Kikubwa cha Teknolojia ya Madini Mkakati, sambamba na ununuzi wa vifaa vya kisasa vya utafiti wa kina wa rasilimali madini.
Akizungumza Januari 26, 2026, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, wakati wa mazungumzo na ujumbe maalum wa wataalam sita kutoka Korea Kusini ulioongozwa na Mtaalam wa Jiolojia na Rasilimali Madini, Seong-Jun Cho kutoka Taasisi ya KIGAM, amesema mradi huo ni sehemu ya mkakati wa Taifa wa kuongeza tija, mapato na uwazi katika sekta ya madini.
Waziri Mavunde amesema maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yameiwezesha Wizara ya Madini kuweka lengo la kuongeza eneo la utafiti wa madini nchini kutoka kiwango cha sasa hadi kufikia asilimia 50 ifikapo mwaka 2030, hatua inayotarajiwa kuchochea uwekezaji, kuongeza mapato ya Serikali na kuboresha upangaji wa miradi ya madini.
“Mradi huu wa ushirikiano kati ya Tanzania na Korea Kusini unaonesha dhamira na azma ya Serikali yetu katika kufikia malengo ya Madini Vision 2030 kwa vitendo,” amesema Waziri Mavunde.

Mradi huo umetokana na makubaliano ya ushirikiano kati ya Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST)na Taasisi ya Jiosayansi na Rasilimali Madini ya Korea (KIGAM) kupitia Hati ya Makubaliano (MoU) iliyosainiwa mwaka 2024. Utekelezaji wake unatarajiwa kuanza mwaka 2027 na kukamilika mwaka 2031, ikiwa ni mpango wa miaka mitano unaolenga hasa madini ya nikeli na madini ya metali nyingine.
Kwa mujibu wa Waziri Mavunde, mradi huo unatarajiwa kugharimu Woni bilioni 21.8 za Korea, sawa na Dola za Kimarekani milioni 16.5, fedha zitakazotumika katika ujenzi wa Kituo cha Teknolojia ya Madini, uanzishaji wa mfumo wa kidijitali wa taarifa za rasilimali madini, ujenzi wa uwezo wa wataalam wa ndani pamoja na utekelezaji wa mifumo ya kimazingira, kijamii na kiutawala (ESG) katika sekta ya madini.
Kupitia kituo hicho cha teknolojia, Serikali inalenga kuboresha upatikanaji wa taarifa sahihi na za kisasa za kijiolojia, jambo litakalowawezesha wachimbaji wadogo, wawekezaji na taasisi za kifedha kufanya maamuzi yenye tija na kupunguza hatari za uwekezaji.
Aidha, Waziri Mavunde ameeleza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza mpango wa kuwawezesha vijana na wanawake katika sekta ya madini (MBT), na kuiomba Taasisi ya KIGAM kushirikiana zaidi katika kujenga uwezo wa rasilimali watu ili kuhakikisha makundi hayo yanashiriki kikamilifu na kunufaika na mageuzi ya sekta ya madini.
“Mradi huu hautaishia kwenye utafiti pekee, bali pia utatoa fursa za mafunzo maalum kwa wachimbaji wadogo ili kuongeza ufanisi, tija na usalama wa shughuli zao,” ameongeza Waziri Mavunde.
Awali, akitoa wasilisho kuhusu mradi huo, Msimamizi Mkuu wa KIGAM, Seong-Jun Cho, ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano mzuri na kuahidi kuwa utekelezaji wa mradi huo utaimarisha mchango wa sekta ya madini katika uchumi wa Taifa, hususan katika kuongeza mapato, ajira na ushindani wa Tanzania katika soko la kimataifa la madini.
Kwa ujumla, mradi huu ni ushahidi wa utekelezaji wa vitendo wa Dira ya Madini 2030, unaolenga kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha utafiti wa madini, matumizi ya teknolojia ya kisasa na ukuaji endelevu wa mapato ya Taifa.


