Na Mwandishi Wetu, Gazetini
MZEE Benson Gabriel Mwakilembe, maarufu kwa jina la Tall, ni miongoni mwa wachimbaji wa madini waliogeuza changamoto kuwa fursa. Baada ya miongo kadhaa akijishughulisha na uchimbaji wa dhahabu, leo hii amesimama kama mmoja wa wamiliki wa Kiwanda cha Kwanza cha Kisasa cha Kuchenjua Shaba nchini – Mineral Access Systems Tanzania Ltd (MAST), kilichopo Chunya, Mkoa wa Kimadini wa Mbeya.
Akizungumza na Madini Diary hivi karibuni, Mzee Mwakilembe alieleza safari yake ndefu kutoka kwenye migodi ya dhahabu hadi kwenye uwekezaji wa teknolojia ya kisasa ya kuchenjua shaba. Anasema uamuzi huo ni matokeo ya kuona fursa kubwa iliyopo katika rasilimali za shaba nchini Tanzania.
“Mimi kwenye dhahabu sirudi tena – sasa niko kwenye shaba. Tanzania tuna shaba nyingi kushinda hata Zambia! Serikali na wachimbaji waione kama zao kuu la biashara, masoko yapo,” anasema kwa kujiamini.
Wakati wa uzinduzi wa kiwanda hicho Juni 18, 2025, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, alisema mradi huo umeiweka Tanzania kwenye ramani ya dunia kama mzalishaji wa shaba, sambamba na kutimiza azma ya serikali kuongeza thamani ya madini kabla hayajasafirishwa nje.
Kwa upande wake, Mzee Mwakilembe anakiri kuwa katazo la Serikali la kusafirisha shaba ghafi nje ya nchi lilikuwa chachu ya mageuzi.
“Tuliona linatuumiza kibiashara, lakini sasa limetufikisha hapa. Kwa mara ya kwanza Tanzania tunachenjua shaba hapa nyumbani na tumeweza kusafirisha copper cement zaidi ya tani 200,” anasema.
Mbali na leseni zake za shaba Chunya, anamiliki pia maeneo ya uchimbaji Simanjiro, Tunduru, Mpwapwa na Njombe, ambayo anapanga kuunganisha uzalishaji wake wote katika kiwanda cha MAST. Dira yake ya baadaye ni kuanza kuchenjua shaba kufikia kiwango cha copper cathode — zao la mwisho lenye thamani kubwa zaidi sokoni.
“Madini yamenifaa sana – ninaendesha maisha, nina miradi mingine, sasa nina mabasi mawili ya abiria kutoka Tunduru hadi Mbeya. Nilipotoka na nilipo sasa ni tofauti kabisa… kwa utani nasema, sasa hivi napanda ndege bana – madini yamenivusha, mimi sikubahatika kusoma!”
Mzee Mwakilembe pia anatoa pongezi kwa viongozi wa Wizara ya Madini kwa ushirikiano mkubwa uliomsaidia kufikia mafanikio hayo:
“Kiwanda hiki ni matokeo ya msaada mkubwa wa viongozi wa Wizara. Mhe Biteko alinifundisha kupambana na wawekezaji, Mhe. Mavunde ndiye nguvu ya MAST, Katibu Mkuu Samamba na kijana wangu Rama wa Tume ya Madini – wote wametusaidia sana.”
Mkurugenzi wa MAST, Godfrey Kente, anasema kiwanda hicho kinalenga kuchenjua shaba yenye kiwango cha chini cha asilimia 0.5 hadi 2 na kuiongeza thamani hadi asilimia 75 kupitia teknolojia ya leaching na cementation.
Kente anabainisha kuwa MAST ina mpango wa kujenga viwanda vingine vitatu vya shaba Manyara, Ruvuma na Dodoma, ambapo kila kimoja kitazalisha ajira zaidi ya 500 na kuchangia takribani USD milioni 40 kwa mwaka katika uchumi wa nchi.
Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kimadini Chunya, Mhandisi Laurent Mayala, anasema tangu kuanzishwa Aprili 2025, kiwanda hicho kimezalisha tani 810 za shaba zenye thamani ya Sh10.3 bilioni, ambapo Sh594 milioni tayari zimeingia Serikalini.
MAST ni kampuni ya Kitanzania iliyoanzishwa mwaka 2011, ikiwa ni matokeo ya uwekezaji wa zaidi ya dola milioni 10 za Kimarekani kwa ubia kati ya kampuni ya MAST na MCC kutoka New York, Marekani.
“Serikali kupitia STAMICO ikae na taasisi za fedha – wachimbaji wakopeshwe kwa leseni zenye tafiti. Pia wananchi waelimishwe kuhusu sekta ya madini. Mama ametuletea mashine, lakini ziwafikie wachimbaji wadogo zaidi na gharama za utafiti zipunguzwe,” anasisitiza.
“Watu waliokuwa Chunya miaka ya 1980 wakirudi leo watashangaa – Chunya imebadilika! Serikali imerahisisha sana shughuli za uchimbaji na biashara ya dhahabu,” anasema Mzee Mwakilembe, akihitimisha simulizi yake yenye mafunzo ya uthubutu, uvumilivu na uzalendo wa kiuchumi.


