Na Imani Nathaniel, Gazetini
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ametoa wito kwa viongozi wa dini kutumia lugha ya staha na kuhubiri mshikamano katika kipindi hiki kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo alipokuwa akifungua mkutano maalum wa viongozi wa dini, Chalamila amesema ni muhimu kwa viongozi hao kusoma alama za nyakati wanapozungumza na waumini wao ili kusaidia kutibu mioyo na kudumisha amani.
“Kiongozi wa dini anapaswa kuhubiri amani kila wakati. ikitoweka, si rahisi kuirudisha,” ameongeza.


Naye Tebeti Halisi kutoka Kanisa Halisi, amesema mikutano kama hiyo inapaswa kuwa endelevu kutokana na matukio mengi ya uvunjifu wa amani katika jamii yanayowahusu watu ambao viongozi wa dini ni walezi wao.
“Semina za namna hii zinatupa uelewa na jinsi ya kuwaelekeza watu kutunza tunu ya amani ili Tanzania iendelee kuwa kisiwa cha amani,” amesema.

Akimalizia, Halisi amesisitiza wajibu wa watumishi wa Mungu kuwaelimisha waumini namna bora ya kuwaombea viongozi wa nchi: “Ukimuombea kiongozi unamlinda, na kiongozi akiwa na amani, jamii na taifa kwa ujumla vitakuwa salama,”.


