22 C
New York

Keiko Fujimori: Binti wa dikteta aliyekwepa njia za baba yake

Published:

LIMA, Peru

KEIKO Fujimori ndiye Rais mpya wa Peru na anakuwa mwanamke wa kwanza katika historia ya nchi hiyo ya Kusini mwa Amerika kushika wadhifa huo.

Si jina geni. Keiko ni binti mkubwa wa Rais wa zamani wa Peru, Alberto Fujimori, ambaye utawala wake wa kuanzia mwaka 1990 hadi 2000 uligubikwa na vitendo vya rushwa na ukiukwaji wa kutisha wa haki za binadamu nchini humo.

Kwa upande wake, Keiko aliyezaliwa mwaka 1975, amekuwa kwenye ramani ya siasa za Peru tangu 1994, wakati huo akiwa na binti mdogo wa umri wa miaka 19 tu.

Aidha, umaarufu wake huo ndani na nje ya Peru ulitokana na wazazi wake kuachana, hivyo Rais Fujimori kumtangaza kama ‘First Lady’ wa Taifa la hilo.

Baadaye, Keiko alianza kutengeneza njia zake mwenyewe kwenye siasa, akiingia bungeni kwa mara ya kwanza mwaka 2006, kabla ya kuwa kiongozi wa Chama cha Popular Force.

Mara zote amejaribu kujijengea picha tofauti na aliyokuwa nayo baba yake na hilo linatajwa na wachambuzi wa siasa kumuongezea ushawishi mkubwa.

Hata hivyo, kama ilivyo kwa wanasiasa wengi, kama si wote, Keiko anayo makandokando yaliyowahi kutia doa mwenendo wake.

Mathalan, waendesha mashitaka wa Peru waliwahi kudai kuwa alipata fedha kwa njia zisizo halali kutoka kwa moja ya kampuni za ujenzi za Brazil wakati wa kampeni za urais za mwaka 2011 na 2016.

Mwaka 2018, Keiko aliingia tena kwenye mijadala baada ya kushikiliwa kwa muda na vyombo vya dola kwa shutuma za utakatishaji fedha, ingawa aliachiwa baadaye.

Safari ya kutimiza ndoto ya urais haikuwa rahisi. Kabla ya kufanikiwa mwaka huu (2026), Keiko alishawahi kuwania mara nne kiti hicho.

Mwaka 2011, aliwania na kufika hatua ya marudio (baada ya kukosekana mgombea mwenye asilimia zaidi ya 50 ya kura). Katika Uchaguzi wa raundi ya pili, akazidiwa na Ollanta Humala.

Alijitosa tena mwaka 2016, ambapo pia alifika hadi raundi ya pili, safari hii akipoteza mbele ya Pedro Pablo Kuczynski. Keiko aliongoza katika raundi ya kwanza lakini hakuzidi asilimia 50 ya kura.

Katika Uchaguzi wa mwaka 2021, aligombea tena. Alipambana na Pedro Castillo lakini kama ilivyokuwa awali, Keiko alipoteza tena katika raundi ya pili.

Mwaka 2026, alikumbana na Roberto Sanchez. Uchaguzi ulifika raundi ya pili na safari hii ni Keiko ndiye aliyeshinda na kutangazwa kuwa Rais mpya wa Peru.

Je, ataishi kwenye njia zake zilizowaaminisha raia wa Peru kuwa anafaa kuwaongoza au atakiuka na kufuata nyayo za baba yake?

Related articles

Recent articles