22 C
New York

Kesi kifo cha Tupac bado ya moto

Published:

LOS ANGELES, Marekani

MAHAKAMA mjini Nevada, Marekani, imetaka mahojiano ya mtuhumiwa wa mauaji ya rapa Tupac Shakur, Duane Davis ‘Keffe D’ yawasilishwe kama ushahidi wakati kesi hiyo itakaposikilizwa tena.

‘Keffe D’ (63), anashitakiwa kwa kumuua Tupac katika tukio la kummiminia risasi jijini Las Vegas mwaka 1996 na endapo atakutwa na hatia atahukumiwa kifungo cha maisha (bila haki ya kupata msamaha wa rais).

Kwa upande wake, Mahakama ya Nevada imeitisha mahojiano aliyofanya ‘Keffe D’ akiwa polisi mwaka 2008, ikiamini yatasaidia wakati wa usikilizaji wa kesi ifikapo Agosti 10, 2026.

Katika mahojiano hayo, mtuhumiwa alikiri kuwa yeye na washikaji zake walimuona Tupac usiku huo na kuanza kulifuatilia gari lake hadi walipomfikia kwenye foleni.

Akitaja gari lao kuwa ni Cadillac, anakiri kupitia mahojiano yake na polisi, kwamba alichukua bunduki na kumpa mtu aliyekuwa siti ya nyuma, ambaye ndiye aliyempiga risasi Tupac.

Miongoni mwa wanaotajwa kuwa na ‘Keffe D’ kwenye gari siku hiyo ni mtoto wa dada yake, Orlando Anderson ‘Baby Lane’, ambaye hata hivyo alikana na kisha kufariki miaka miwili tu baada ya kifo cha rapa huyo.

Kwa upande wake, Tupac kwenye gari lake alikuwa na bosi wa lebo maarufu wakati huo ya Death Row Records, Marion ‘Suge’ Knight, ambaye alipata majeraha machache.

Katika hatua nyingine, wakili anayemtetea Keffe D, Michael Sanft, hakubaliani na uamuzi huo wa Mahakama akisisitiza kuwa mahojiano ya mteja wake na polisi yanapaswa kuwa siri.

Related articles

Recent articles