22 C
New York

Italia ya ‘mababu’ Mancini, Ranieri itavuna nini?

Published:

MILAN, Italia

ROBERTO Mancini ameajiriwa na kuikuta timu ya soka ya Taifa ya Italia ikiwa kwenye hali mbaya. Haijafuzu Kombe la Dunia kwa misimu yote mitatu ya hivi karibuni (2018, 2022 na 2026).

Mbali na Mancini mwenye umri wa miaka 61, pia Shirikisho la Soka la Italia (FIGC) limemtangaza kocha aliyewahi kuipa Leicester City ubingwa wa Ligi Kuu ya England, Claudio Ranieri, kuwa Mkurugenzi wa Ufundi.

Ranieri (76), ambaye aliwahi pia kupita Chelsea akiwa kocha, amechukua nafasi ya mkongwe mwenzao, Paolo Maldini, ambaye alidumu kwenye kiti hicho kwa siku 16 tu.

Baada ya Italia kukosa tiketi ya kucheza Kombe la Dunia 2026, aliyekuwa Rais wa FIGC, Gabriele Gravina, alijiuzulu, kama alivyofanya kocha Gennaro Gattuso.

AMERUDI KAMBINI

Kwa upande mwingine, Mancini si kocha mpya katika benchi la ufundi la Azzurri. Baada ya timu hiyo kushindwa kufuzu Kombe la Dunia mwaka 2018, alikabidhiwa mikoba.

Miaka miwili baadaye, Mancini aliweza ‘kuifufua’ Italia na kuipa taji la fainali za EURO, wakiifunga Italia kwa mikwaju ya penalti katika mchezo wa fainali uliochezwa kwenye Uwanja wa Wembley.

Licha ya kushindwa kufuzu Kombe la Dunia mwaka 2022, Italia ilicheza mechi 37 bila kufungwa. Ilishangaza wengi kusikia Mancini anajiuzulu mwaka 2023 na wiki mbili baadaye kujiunga na timu ya Taifa ya Saudi Arabia.

Hata hivyo, kocha huyo wa zamani wa Inter Milan na Manchester City aliachana na Saudi Arabia mwaka 2024 na hivi karibuni alikuwa na klabu ya Al-Sadd ya Ligi Kuu nchini Qatar.

HUYU HAPA RANIERI

Baada ya Mancini kuondoka ghafla mwaka 2023, Shirikisho la Soka la Italia lilimpa kazi Luciano Spalletti aliyekuwa amefanya makubwa akiwa na kikosi cha Napoli.

Hata hivyo, ilimchukua miaka miwili tu, akatimuliwa kwenye benchi baada ya Italia kufungwa na Norway katika mchezo wa kwanza wa kufuzu fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2026.

Kama itakumbukwa, Ranieri alifuatwa ili kwenda kuziba pengo la Spalletti lakini aligomea ofa, hivyo Shirikisho likamgeukia Gattuso na kumuajiri.

Kwa hivi karibuni, alikuwa mshauri katika klabu ya AS Roma. Aliondoka klabuni hapo Aprili, 2026, baada ya kukorofishana na kocha Gian Piero Gasperini.

GUARDIOLA, ANCELOTTI WALIGOMA

Kabla ya kumpa kazi Mancini, Shirikisho liliwafikia na kufanya mazungumzo na makocha wakubwa watatu – Pep Guardiola, Carlo Ancelotti na Antonio Conte – lakini wote waligoma kwa nyakati tofauti.

Hivyo, ilionekana wazi kuwa kibarua hicho kingetua kwa mkongwe Andrea Pirlo. Siku chache zilizopita, waliachana na jina lake kutokana na shinikizo la wanasiasa nchini Italia, ambao wakisema hafai kwa kuwa ni balozi wa moja ya kampuni za Urusi.

Hiyo ilikuwa ni sababu ya kisiasa, ikizingatiwa kuwa Urusi imetengwa na mataifa ya Ulaya, ikiwamo Italia, kwa kitendo chake cha kuivamia kijeshi Ukraine.

Hatua hiyo ya ‘kumpotezea’ Pirlo haikumfurahisha Maldini na ndiyo inayotajwa kusababisha ajiuzulu nafasi yake ya Ukurugenzi wa Michezo.

ITALIA MPYA?

Ni swali la msingi na gumu kuelekea maisha mapya ya timu ya Taifa ya Italia chini ya Mancini. Mechi yake ya kwanza ni ile ya Septemba, 2026, dhidi ya Ubelgiji.

Mechi yake ya pili itachezwa Oktoba, 2026, ambapo wataivaa Uturuki, kabla ya kuikabili Ufaransa. Michezo yote mitatu ni ya Ligi ya Mataifa ya Ulaya (UEFA Nations League).

Timu zote hizo zilikuwa kwenye michuano ya Kombe la Dunia ya mwaka huu na mbili ziliweza kufika hatua ya robo fainali.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotangazwa na Shirikisho, Mancini atakuwa na vipindi viwili vya mazoezi na timu ya taifa kabla ya mchezo wao wa kwanza (dhidi ya Ubelgiji).

Related articles

Recent articles