23.2 C
New York

Utafiti mpya wa Shanta Gold waongeza matumaini ya dhahabu zaidi Chunya

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetii- Chunya

UPANUZI wa shughuli za uchimbaji uliofanyika katika eneo la Porcupine North umeongeza uhai wa Mgodi wa Shanta Gold – New Luika kwa miaka mitano zaidi, kutoka mwaka 2029 hadi kufikia 2034. Aidha, kupitia utafiti unaoendelea, mgodi huo unatarajia kuongeza zaidi shughuli za uchimbaji wa madini ya dhahabu.

Hayo yalibainishwa Oktoba 7, 2025, na Kaimu Meneja Mkuu wa Mgodi wa Shanta Gold – New Luika, Mhandisi Ladislaus Kwesigabo, wakati akizungumza na timu ya Madini Diary iliyotembelea mgodi huo kwa lengo la kujionea maendeleo ya shughuli za uchimbaji na mchango wake katika kukuza uchumi wa wilaya ya Chunya na taifa kwa ujumla.

Kwesigabo alisema kuwa baada ya upanuzi wa eneo hilo, shughuli za uzalishaji zinaendelea vizuri na kampuni inaendelea na tafiti zaidi kupitia leseni nyingine inazomiliki ili kuongeza uhai wa mgodi huo.

Mnamo Aprili 3, 2025, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, alizindua rasmi shughuli za uchimbaji katika mgodi wa Porcupine North uliopo kata ya Mkola, Makongolosi, wilayani Chunya. Eneo hilo lilitokana na leseni hodhi zilizorejeshwa serikalini kwa mujibu wa sheria baada ya kumalizika kwa shauri la kimahakama na mwekezaji wa awali, ambapo Serikali iliweka utaratibu wa kumpata mwekezaji mpya kwa uwazi, na kampuni ya Shanta Mining Company Limited ilishinda zabuni hiyo.

Mgodi wa New Luika unamilikiwa na kampuni ya Kitanzania, Shanta Mining Company Limited, iliyoanzishwa mwaka 2001. Kampuni hiyo ilianza utafiti wa madini mwaka 2004 na kuanza uchimbaji mwaka 2010, kabla ya dhahabu ya kwanza kuzalishwa mwaka 2012. Tangu wakati huo, kampuni imeendelea na shughuli za uchimbaji kwa wastani wa uzalishaji wa wakia 55,000 hadi 60,000 kwa mwaka.

Kwa mujibu wa Mhandisi Kwesigabo, mgodi huo umeajiri asilimia 99 ya Watanzania, wakiwemo asilimia 40 kutoka maeneo yanayozunguka mgodina asilimia 60 kutoka sehemu nyingine za Tanzania. Aidha, asilimia 70 ya kampuni zinazotoa huduma na bidhaa kwa mgodi huo ni kampuni za Kitanzania zinazojihusisha na uchimbaji, usafirishaji na huduma nyingine muhimu.

“Fursa za kutoa huduma kwenye mgodi wetu zipo. Ili ufanye kazi na Shanta lazima uwe umesajiliwa kihalali, na taratibu zetu zote zinafanyika kwa uwazi,” alisema Mhandisi Kwesigabo.

Aliongeza kuwa mgodi huo unatoa nafasi za ajira kwa wanawake katika nyanja mbalimbali kama utafiti, uendeshaji mitambo na uhandisi.

Kuhusu ushiriki wa mgodi katika shughuli za kijamii, alisema kampuni imewekeza kwenye huduma za afya, elimu, maji, kilimo na miradi ya kuwaandaa wananchi kunufaika hata baada ya mgodi kufungwa.

Aidha, alisema shughuli za uchimbaji mdogo wilayani Chunya zimeendelea kukua kwa kasi ukilinganisha na miaka mitano iliyopita, kutokana na ongezeko la bei ya dhahabu.

Hata hivyo, alibainisha kuwa changamoto kubwa iliyopo ni baadhi ya wachimbaji wadogo kuingia kwenye maeneo ya leseni za kampuni au za wachimbaji wengine, akitoa wito kwao kuzingatia sheria na mipaka ya leseni.

Uwepo wa mgodi wa Shanta Gold – New Luika umeendelea kuchochea maendeleo ya kiuchumi kupitia ajira, mapato kwa serikali na utekelezaji wa miradi ya kijamii (CSR) katika mikoa ya Songwe na Mbeya (Chunya).

Mbali na mgodi wa New Luika, kampuni ya Shanta pia inamiliki mgodi wa Singida Gold Mine uliopo mkoani Singida.

Related articles

Recent articles