WASHINGTON DC, Marekani
WAZIRI Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, alikuwa nchini Marekani kwa ziara ya kikazi, ambapo alikutana na kufanya mazungumzo na Rais Donald Trump.
Kwa upande mwingine, ziara hiyo imetafsiriwa kuwa ni jitihada zake za ‘kufufua’ uhusiano ulioyumba kwa sasa kati yake na Marekani.
Utafiti wa hivi karibuni na majibu yake kutolewa Julai 28, 2026, umeonesha kuwa asilimia 49 ya raia wa Marekani wanataka Netanyahu akamatwe akiwa nchini kwao na kukabidhiwa ICC.
ICC, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, imetoa kibali cha kukamatwa kwa Netanyahu ili kujibu mashitaka ya uhalifu dhidi ya binadamu huko Gaza.
Kwamba wengi wao wanaamini kuwa Waziri Mkuu huyo anahusika moja kwa moja na anastahili kupandishwa mahakamani mjini The Hague.
Uhusiano wa Netanyahu na Marekani ulianza kuyumba tangu alipojiingiza katika siasa za Marekani kwa kuchagua upande wa Chama cha Republican.
Kwa miaka mingi, Israel haijawahi kuwa mfuasi wa Chama kimoja, na badala yake kiliungwa mkono na vyote viwili; Republican na Democrats.
Alifanya kosa mwaka 2015 baada ya kukubali mwaliko wa Republican katika kikao cha kuijadili Iran juu ya nyuklia, wakati huo Rais wa Marekani akiwa Barack Obama.
Kwa kufanya hivyo, Netanyahu alijijengea uadui mbele ya wafuasi wa Democrats, ambao waliona kwamba kwa mara ya kwanza, Israel imechagua upande katika siasa za Marekani.
Wakati wa utawala wa Rais Joe Biden, licha ya wanasiasa wa Democrats kukosoa, Serikali yake iliendelea kuiunga mkono Israel, ikiisaidia kijeshi, kisiasa na kidiplomasia katika uhalifu dhidi ya Wapalestina.
Democrats walikosoa hatua ya Biden kuitembelea Israel wakati huo, pia kutetea ndani ya Marekani na hata katika vikao vya Umoja wa Mataifa (UN).


