HAVANA, Cuba
KWA miaka mingi, Cuba imekuwa ikisifika kwa ubora wa sekta yake ya afya, huku raia wake wakifurahia huduma ya matibabu bila malipo kwa Serikali kubeba gharama zote.
Hata hivyo, kwa sasa mambo yamebadilika na sekta ya afya nchini Cuba iko hoi, au ‘ICU’, kama unavyoweza kuifananisha na mgonjwa anayehitaji uangalizi maalumu.
Ndiyo, licha ya huduma za afya kuendelea kutolewa bure na Serikali kubeba mzigo wa gharama, upatikanaji wake na hata ubora umeshuka kwa kiasi kikubwa.
Kwa upande mwingine, wataalamu wa afya nchini humo wanauona mustakabali mbaya wa sekta hiyo, wakitaja uhaba wa dawa na kuongezeka kwa idadi ya vifo kuwa ni changamoto kubwa kwa sasa.
Nini chanzo cha tatizo? Ni vikwazo ilivyowekewa na Marekani. Miezi sita iliyopita, yaani Januari 29, 2026, Rais wa Marekani, Donald Trump, alitangaza kuzuia meli za mafuta kuingia Cuba.
Rais Trump alienda mbali zaidi akizionya nchi zinazofanya biashara ya mafuta na Cuba kuacha mara moja, kabla hazijaingia kwenye orodha ya maadui wa Marekani.
Lengo ni kuipa wakati mgumu Serikali iliyoko madarakani, ambayo Rais Trump amekuwa akiita kuwa ni tishio kwa usalama wa Kisiwa hicho.
Tangu katazo hilo, Cuba imepokea meli moja pekee ya mafuta, hivyo kufanya hali ya kiuchumi kuwa mbaya katika Taifa hilo.
Aidha, kutokana na uhaba wa nishati ya mafuta, nchi hiyo imejikuta gizani kutokana na kukosa umeme wa uhakika, ambapo hukatika kwa hadi saa 20 kwa siku.
Kuhusu sekta ya afya, hali imeonekana kuwa mbaya zaidi. Si tu kukatika kwa umeme mara kwa mara, bali pia hospitali nyingi zinakabiliwa na uhaba wa dawa.
Kampuni za Ulaya za usambazaji wa dawa na vifaa-tiba hazifanyi biashara na Cuba zikihofia vikwazo vya Marekani, ikiwamo kupandishiwa tozo.
Kampuni kubwa mbili za meli za Hapag-Lloyd na CMA CGM zilisitisha kufanya kazi na Cuba, ikiwa ni katika kutii amri hiyo ya Rais Trump.
Kwa upande mwingine, watoto nchini Cuba ndiyo wahanga wakubwa wa hicho kinachoendelea. Wastani wa watoto wenye saratani kupona umeshuka kutoka asilimia 85 hadi 65.
Pia, wakati Trump anaingia madarakani kwa mara ya kwanza mwaka 2017, Cuba ilikuwa na wastani wa vifo vinne katika kila watoto 1,000 wanaozaliwa. Kwa sasa, idadi imepanda na kufikia watoto 9 katika kila 1,000.
“Watoto wanapoteza maisha kwa sababu madaktari hawana vifaa na dawa,” anasema Kamishina wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa (UN), Volker Turk.
Turk alienda mbali zaidi na kuiomba Marekani kulegeza vikwazo dhidi ya Cuba, akisistiza kuwa kinachoendelea kwa sasa hakikubaliki. “Hii hakikubaliki kabisa,” aliongeza.
Vilevile, idadi ya vifo vinavyotokana na uzazi navyo vimepanda kwa wastani wa 44.1 katika kila akina mama 100,000, ikilinganishwa na 40.6 mwaka 2024.
Katika baadhi ya hospitali kubwa, malalamiko ya madaktari kuchelewa kufika kazini kutokana na changamoto ya usafiri, nayo imeripotiwa.
Kwa miaka zaidi ya 60, Cuba imekuwa ‘ikiogelea’ kwenye machungu ya vikwazo vya Marekani lakini hali imekuwa mbaya zaidi tangu Rais Trump alipoingia madarakani, kuanzia mwaka 2017, kisha muhula wake wa pili mwaka 2025.


