25.3 C
New York

Lula kushinda tena kiti cha urais Brazil?

Published:

RIO, Brazil

RAIS wa Brazil, Luiz Inacio Lula da Silva, ameanza rasmi kampeni zake za kuwania muhula wa nne kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao wa Oktoba, 2026.

Kupitia Workers’ Party (Chama cha Wafanyakazi), Lula mwenye umri wa miaka 80 alirejea madarakani mwaka 2023 baada ya kuiongoza Brazil kwa mihula miwili kuanzia mwaka 2003 hadi 2010.

Katika Mkutano wake wa kwanza wikiendi iliyopita, mwanasiasa huyo aliwaahidi wafuasi wake kuwa anakwenda kushinda tena kiti cha urais na kurudi Ikulu kumalizia muhula wake.

AHADI ZAKE

Lula ameahidi kuongeza bajeti kwenye ulinzi na usalama, pia kulinda rasilimali za Brazil ili kuhakikisha haziwi mikononi mwa mataifa ya nje.

Katika hilo, Lula amezionya China, Marekani na Ufaransa, akisema hazitoruhusiwa kuingia na kuchota madini ya Brazil.

“Nimejipanga kuhakikisha Brazil haivamiwi na inaheshimiwa,” alisema katika mkutano wake wa kwanza mjini Sao Paulo.

UHUSIANO WAKE NA MAREKANI

Kwa siku za hivi karibuni, Serikali ya Lula imekuwa na uhusiano usio na afya kati yake na utawala wa Rais wa sasa wa Marekani, Donald Trump.

Julai, 2026, Serikali ya Marekani ilitangaza tozo kwa bidhaa za Brazil zinazoingia nchini humo, ikifanya hivyo mara mbili kwa nyakati tofauti.

Marekani inaishutumu Brazil kwa kukiuka sheria za kibiashara kati ya nchi hizo, jambo ambalo Serikali ya Lula imekanusha mara zote.

MPINZANI WAKE

Wakati huo huo, Rais Trump amekuwa akimuunga mkono mpinzani mkubwa wa Lula katika Uchaguzi wa mwaka huu, Seneta Flavio Bolsonaro, ambaye ni mtoto wa Rais wa zamani wa Brazil, Jair Bolsonaro.

Bolsonaro (45), ameibuka baada ya baba yake kushitakiwa kwa kosa la uhaini, akitajwa kutaka kumzuia Lula kuingia madarakani baada ya Uchaguzi uliopita (2022).

Hata hivyo, katika utafiti uliofanywa hivi karibuni na taasisi ya Datafolha, Lula ameonekana kuwa na asilimia 48 ya kushinda, huku Flavio akiwa na asilimia 43.

Tofauti hiyo ndogo inaufanya Uchaguzi huo kutarajiwa kuwa na ushindani mkali, hivyo kuongeza presha kwa Lula anayetaka kutetea kiti chake.

CHANGAMOTO ZA NDANI

Katika mambo anayoweza kujivunia Lula kuelekea siku ya Uchaguzi ni kukua kwa uchumi na hata ongezeko kubwa la nafasi za ajira. Amefaulu katika hayo.

Lakini, Wabrazil wanalalamikia kupanda kwa gharama za maisha, pamoja na changamoto za usalama kutokana na wimbi la magenge ya uhalifu.

Sambamba na hayo, pia zipo kelele za kukithiri kwa vitendo vya rushwa, ambapo Lula na hata Flavio wanatajwa kujipatia fedha za kampeni kwa njia zisizo halali.

AJITETEA ISHU YA UMRI

Kwa upande mwingine, wakosoaji wa Lula wanasema kwa umri wa miaka 80 alionao mwanasiasa huyo, alipaswa kupumzika na kuwaachia vijana wenye nguvu na fikra zinazoendana na kasi ya mabadiliko ya dunia.

Hata hivyo, katika Mkutano wake wa kwanza, Lula alipuuza hoja hiyo na kuwajibu akisema hajioni kama amepoteza nguvu ya kuiongoza Serikali.

Alidai kuwa kutembea na kufanya mazoezi ya viungo kumemfanya ajione imara zaidi kuliko alivyowania na kushinda Uchaguzi wa mwaka 2002.

Related articles

Recent articles