26.8 C
New York

Aisha Mohamed: Kutoka Mhasibu hadi kuiongoza GSM Group

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

KUNA msemo unaosema, “Viongozi wakubwa hawazaliwi, hujengwa.” Katika ulimwengu wa biashara, kauli hiyo inajidhihirisha kupitia watu wanaoanza katika nafasi za kawaida, hujifunza kwa bidii, hukubali changamoto na baadaye hupewa jukumu la kuamua mustakabali wa taasisi kubwa.

Safari ya Aisha Mohamed ni mfano halisi wa falsafa hiyo. Leo hii anahudumu kama Kaimu Mtendaji Mkuu (Ag Group CEO) wa GSM Group, moja ya makundi makubwa ya biashara nchini Tanzania. Lakini nyuma ya nafasi hiyo kuna miaka ya kujifunza, kufanya maamuzi magumu ya kifedha, kusimamia uwekezaji wa mamilioni ya dola na kujenga uwezo wa kuongoza watu na biashara kwa wakati mmoja.

Ni safari inayobeba ujumbe kwamba mafanikio makubwa hayatokani na kupanda cheo kwa haraka, bali kujenga msingi imara wa taaluma, maarifa na uadilifu.

Elimu iliyofungua milango ya mafanikio.

Aisha alichagua kujijengea msingi imara wa taaluma kabla ya kutafuta nafasi za uongozi.

Mwaka 2011 alihitimu Shahada ya Sayansi katika Uhasibu (Bachelor of Science in Accounting) kutoka Minnesota State University Moorhead nchini Marekani. Mbali na masomo, alijihusisha na shughuli za uongozi na kijamii kupitia vikundi vya wanafunzi, jambo lililomjengea uwezo wa kushirikiana na watu kutoka tamaduni mbalimbali.

Hakutosheka na hapo.

Mwaka 2015 alipata Shahada ya Uzamili (MSc) katika Business Analytics and Decision Sciences kutoka University of Leeds nchini Uingereza kwa daraja la Distinction, mafanikio yanayoonyesha kiwango cha juu cha umahiri wa kitaaluma.

Katika zama ambazo biashara zinaendeshwa kwa nguvu ya taarifa na takwimu, elimu hiyo ilimpa uwezo wa kutumia uchambuzi wa data katika kufanya maamuzi ya kimkakati, kutathmini uwekezaji na kuboresha utendaji wa biashara.

Kwa lugha rahisi, alijifunza si tu namna ya kuhesabu fedha, bali namna ya kuzifanya fedha zifanye kazi.

Aisha Mohamed.

Mwanzo mdogo uliokuja kuwa msingi mkubwa

Kama ilivyo kwa wataalamu wengi waliofanikiwa, Aisha hakuanza akiwa mtendaji mkuu.

Alianza kama Accounting Assistant nchini Marekani, akijifunza misingi ya nidhamu ya fedha, uwajibikaji na mifumo ya ndani ya taasisi.

Baadaye alijitolea kupitia programu ya Volunteer Income Tax Assistance (VITA), akisaidia familia na wafanyabiashara wadogo kuandaa marejesho ya kodi.

Uzoefu huo ulimfundisha jambo ambalo halifundishwi darasani—kwamba taaluma bora huanza kwa kuhudumia wengine.

Aliporejea Tanzania mwaka 2012, alianza tena kutoka ngazi za chini kama Junior Accountant kabla ya kuhamia Africa Logistics Solutions Ltd, ambako alijifunza kwa vitendo jinsi fedha zinavyohusiana na biashara za kimataifa, usafirishaji na matumizi ya teknolojia katika uendeshaji wa kampuni.

GSM: Mahali alipojijenga kuwa kiongozi

Mwaka 2015 ndipo ukurasa mpya ulipofunguliwa.

Aisha alijiunga na GSM Group akiwa Group Head of Treasury, akisimamia ukwasi wa kampuni, mikopo, uwekezaji na usimamizi wa hatari za kifedha kwa kampuni nyingi zilizokuwa chini ya kundi hilo.

Lakini hakubaki kwenye eneo moja.

Alipewa pia jukumu la kusimamia fedha za miradi mipya kama Project Finance Lead, ambapo aliongoza maandalizi ya kifedha ya zaidi ya miradi 24 yenye thamani ya zaidi ya dola milioni tisa za Marekani.

Kwa upande wa mali, alisimamia zaidi ya majengo 30 ya biashara, makazi na viwanda vya GSM, huku akishiriki kupata mkopo wa dola milioni 3.5 kwa ajili ya ujenzi wa jengo jipya la biashara pamoja na kusimamia miradi ya ujenzi yenye thamani ya zaidi ya dola milioni 11.

Haya siyo mafanikio ya mtu aliyekuwa akifanya kazi ya kuhesabu fedha pekee.

Ni ushahidi wa mtu aliyekuwa akijifunza jinsi fedha zinavyoweza kuwa nyenzo ya kukuza biashara.

Kutoka mtaalamu wa fedha hadi mwanamkakati wa biashara

Kadiri miaka ilivyokwenda, jukumu lake ndani ya GSM lilianza kubadilika.

Badala ya kuulizwa fedha zinapatikanaje, alianza kuulizwa biashara inapaswa kwenda wapi.

Mwaka 2023 aliteuliwa kuwa Head of Strategy & Projects, akiongoza uandaaji wa mkakati wa kampuni, kuratibu miradi ya kimkakati na kusaidia kuweka dira ya ukuaji wa GSM.

Baada ya muda mfupi, alikabidhiwa jukumu kubwa zaidi la kuongoza Kitengo cha Logistics, kilichokuwa na kampuni nane na wafanyakazi zaidi ya 1,800 waliokuwa wakihudumia bandari tano kubwa barani Afrika.

Hapo ndipo alipoonyesha uwezo wa kuunganisha taaluma ya fedha na uongozi wa watu.

Alisimamia matumizi ya teknolojia kuboresha ufanisi, kupunguza gharama na kuanzisha huduma mpya zilizolenga kuongeza mapato ya biashara.

Hatua ya mwisho kuelekea kileleni

Mwaka 2025 aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Miradi na Uwekezaji, akisimamia uwekezaji wa GSM katika sekta za majengo, miundombinu na biashara mpya.

Katika nafasi hiyo, aliongoza mchakato mzima wa miradi, kuanzia upembuzi yakinifu, upangaji wa mtaji, utekelezaji hadi kukabidhi miradi iliyokamilika.

Uzoefu huo ulimwandaa kwa jukumu kubwa zaidi.

Kuanzia Januari 2026, Aisha alikabidhiwa nafasi ya Kaimu Mtendaji Mkuu wa GSM Group, akisimamia mkakati wa kundi, uwekezaji, utendaji wa biashara mbalimbali, miradi mikubwa ya maendeleo pamoja na usimamizi wa hatari na utawala bora.

Ni nafasi inayomweka miongoni mwa wanawake wachache wanaoongoza makundi makubwa ya biashara nchini Tanzania.

Somo ambalo vijana wanaweza kujifunza

Safari ya Aisha Mohamed inatoa fundisho muhimu kwa vijana wengi wanaotamani kufanikiwa katika sekta ya biashara.

Kwanza, hakuna kazi ndogo ikiwa inaleta maarifa. Alianza kama mhasibu wa kawaida kabla ya kuwa mtendaji mkuu.

Pili, elimu ni uwekezaji unaolipa. Aliongeza thamani yake kwa kujifunza uhasibu, kisha akaenda hatua nyingine kwa kusomea Business Analytics katika kipindi ambacho matumizi ya data yamekuwa msingi wa maamuzi ya biashara duniani.

Tatu, ukuaji wa kweli unahitaji kujifunza kila hatua. Badala ya kubaki kwenye eneo moja la utaalamu, alijifunza fedha, uwekezaji, usimamizi wa mali, mikakati ya biashara na uongozi wa watu.

Na mwisho, mafanikio makubwa hujengwa kwa uvumilivu. Safari yake ya takribani miaka 15 inaonyesha kuwa nafasi za juu haziji kwa bahati, bali kwa maandalizi, matokeo na uwezo wa kujenga imani kwa wale unaowaongoza.

Related articles

Recent articles