Na Hassan Mwasha, Gazetini
ACHANA na ishu ya ubingwa. Ni wazi si Yanga wala Simba inayoweza kufikia idadi ya pointi ilizokusanya msimu uliopita (2024-25) wa Ligi Kuu Bara.
Kwa sasa, Yanga iko kileleni mwa msimamo lakini imekusanya pointi 72, wakati Simba wao wana pointi 70, huku kila timu ikiwa imebakiza mechi moja baada ya kucheza 29.
Hivyo, endapo Yanga itaifunga JKT katika mchezo ujao wa Juni 30, 2026, itamaliza msimu ikiwa na pointi 75.
Kwa Simba, hata kama itapata ushindi mbele ya KMC katika mchezo wa mwisho utakaochezwa siku hiyo, itafunga msimu ikiwa na pointi 73.
Ni tofauti na ilivyokuwa msimu uliopita, 2024-25, ambapo Yanga ilitwaa ubingwa ikiwa na pointi 82 katika mechi 30.
Simba, kwa upande wao, walimaliza msimu huo wakiwa na nafasi ya pili kwenye msimamo lakini walikusanya pointi 78.


