MIAMI, Marekani
MWAKA 2022, Morocco ilikuwa timu ya kwanza ya Afrika kufikia nusu fainali katika historia ya michuano ya Kombe la Dunia.
Safari hii, kwa maana ya fainali zinazoendelea huko Marekani, Mexico na Canada, Afrika ilipeleka wawakilishi 10.
Kati ya hao, tisa wameweza kuvuka makundi na kuingia hatua ya 32 Bora. Ni Tunisia pekee iliyorudi nyumbani.
Ivory Coast ilimaliza nafasi ya pili Kundi E na hii ni mara yake ya kwanza kuvuka makundi katika historia ya Kombe la Dunia.
Afrika Kusini nayo ilimaliza nafasi ya pili katika Kundi A na hii pia ni mara ya kwanza kwao kuvuka hatua ya makundi kwenye michuano hiyo.
Morocco walimaliza katika nafasi ya pili kwenye kundi lao, kama ilivyokuwa kwa Misri iliyokuwa Kundi G.
Senegal, baada ya ushindi mnono wa mabao 5-0 dhidi ya Iraq, imeingia kupitia ‘best Loser’, licha ya kushika nafasi ya tatu kwenye kundi lake.
Ghana nao walivuka makundi wakiwa na mechi moja mkononi, wakati Cape Verde nao waliingia 32 Bora baada ya sare katika mechi zote tatu dhidi ya Hispania, Uruguay na Saudi Arabia.
Cape Verde, nchi yenye watu 500,000, imevuka makundi, licha ya kwamba hii ni mara yake ya kwanza kucheza Kombe la Dunia.


