28.1 C
New York

Unamsaidiaje mtoto wako kuchagua tahasusi Kidato cha Tano?

Published:

Na Hassan Mwasha, Gazetini

HIKI ni kipindi ambacho wazazi wako ‘bize’ na maandalizi ya shule kwa wanafunzi wanaokwenda kuianza safari ya elimu kwa masomo ya Kidato cha Tano nchini. Mwaka wa Masomo utaanza Julai, 2026.

Ubize unatofautiana kati ya wazazi ambao watoto wao wamepangiwa shule za maeneo jirani na wale watakaolazimika kuhama mkoa mmoja na mwingine.

Kwa watakaolazimika kusafirisha watoto, wao mambo ni mengi, kubwa ikiwa ni suala la gharama.

Hata hivyo, mara nyingi maandalizi ya wazazi kwa wanafunzi wa Kidato cha Tano hujikita katika ununuzi wa sare, vitabu/madaftari, na nauli au fedha za kujikimu kwa wanafunzi wa mbali.

Hivyo, wazazi wengi huwa hawajishughulishi kabisa na suala la tahasusi (combination) walizochaguliwa au walizochagua watoto wao.

Ilimradi tu mtoto amechaguliwa na Serikali au amebadili na kuchagua tahasusi, basi aende tu akasome. Ni kosa!

Ni katika mazingira ya aina hiyo, baadhi ya watoto hukosa muongozo, hivyo kuchagua tahasusi kwa msukumo wa marafiki au sababu zingine zisizo na weledi.

Hapo wengi wao hujikita wakichagua au kuchaguliwa tahasusi ambazo hazilengi moja kwa moja ndoto walizonazo.

Kama si hivyo, wakati mwingine hujikuta katika tahasusi ambazo haziendani na uwezo wao darasani.

Matokeo yake, hujikuta wakishuka kitaaluma, tofauti na walivyokuwa Kidato cha Nne, na mwishowe kufeli mtihani wa mwisho wa Kidato cha Sita.

Mzazi, kwa nafasi yake, anapaswa kukaa, kuzungumza na kujadili na mtoto juu ya tahasusi aliyochaguliwa au aliyoichagua.

Tofauti na wengi wanavyofikiri, kusimamia na kumpa mtoto wako muongozo wa tahasusi inayomfaa haina uhusiano na mzazi kuwa msomi. Ni suala la kujitambua tu.

Mathalan, kwa kuwasiliana na walimu wa shule alikomaliza mtoto kidato cha nne, wanaweza kuwa na muongozo mzuri wa tahasusi kwa mtoto kutokana na kuujua vizuri uwezo wake katika masomo.

Pia, kwa kuwashirikisha ndoto ya mtoto, wao wanaweza kumpa muongozo wa tahasusi sahihi ya kuiendea, wakioanisha na uwezo aliokuwa nao darasani.

Msistizo; maandalizi ya watoto kwenda Kidato Cha Tano, mwaka wa masomo ukitarajiwa kuanza Julai, 2026, yanapaswa kugusia pia masuala ya kitaaluma, badala ya kujikita tu katika ununuzi wa vifaa vya shule.

Kila la kheri ‘njuka’ wa Kidato cha Tano kwa Mwaka wa Masomo 2026-27.

Related articles

Recent articles