Na Hassan Mwasha, Gazetini
MSIMU wa 2025-26 wa Ligi Kuu Bara uko ukingoni, huku timu nne za juu zikitarajiwa kubaki vilevile kama ilivyokuwa msimu uliopita (2024-25).
Kuelekea Juni 30, 2026, siku ya kumalizika kwa msimu, Yanga iko kileleni, ikifuatiwa na Simba, Azam, na Singida Black Stars.
Baada ya kila timu kushuka dimbani mara 29, Yanga imekusanya pointi 72, Simba ina 70, Azam inafuata ikiwa na pointi 61, kisha Singida Black Stars yenye 50.
Ukiacha Yanga na Simba zinazoweza kubadilishana nafasi kutokana na matokeo ya mechi za mwisho, Azam na Singida Black Stars zitabaki nafasi ya tatu na ya nne.
Ni kwa sababu Azam haitaweza kufikia pointi 70 ili kuishusha Simba iliyo juu yake, kama ambavyo Singida haitoweza kufikisha pointi 61 walizonazo matajiri hao wa Chamazi.
Wakati huo huo, msimamo huo hautofautiani na ule wa msimu uliopita, 2024-25, ambapo ulikuwa na Yanga (pointi 82), Simba (78), Azam (63), kisha Singida (57) katika nafasi ya nne.


