Na mwandishi wetu, Gazetini
KATIKA sehemu ya tatu ya mfululizo wa makala haya, tuliona Lungu akirejea katika nafasi yake ya Rais wa PF baada ya Miles Sampa aliyekuwa akivutana naye kukubali yaishe mwaka 2025. Endelea kusoma …
Lungu, baba wa watoto sita katika ndoa yake na bi. Esther Lungu aliyemuoa mwaka 1986, kwa wakati wote huo wa harakati zake za siasa, alikuwa na historia ya kusumbuliwa na maradhi.
Katika tukio la Juni, 2021, Lungu alianguka ghafla wakati wa hafla ya kijeshi iliyokuwa ikirushwa mubashara kupitia vituo vya televisheni.
Pia, mwanzoni mwa mwaka 2025, alipelekwa Afrika Kusini kwa matibabu, ingawa ugonjwa uliokuwa ukimsumbua haukutajwa, kabla ya gwiji huyo wa siasa kufariki Juni 5 akiwa huko huko.
Baada ya taarifa hizo, Zambia ilitangaza siku saba (wiki moja) ya maombolezo, huku majirani zao, Msumbiji, wakiweka siku tatu.
Februari 5, 2026, taarifa zisizo rasmi zilidai kuwa binti wa Lungu amesema baba yake alipewa sumu akiwa kwenye matibabu mjini Pretoria.
Hata hivyo, haikuchukua muda mrefu, familia iliibuka na kukanusha taarifa hizo kupitia kwa kampuni ya uwakili ya Mashele Attorneys ya Afrika Kusini.
“Familia itashirikiana katika uchunguzi wa kijinai lakini inasisitiza kuwa madai hayo ni uzushi na yanakosa ushahidi,” ilieleza taarifa ya familia.
Aidha, wakati wote huo, familia iliendelea kusisitiza kuwa inataka kumzika Lungu na si Serikali ya Zambia kukabidhiwa mwili, kama ambavyo hufanywa kwa viongozi wengine.
Ilitaka Lungu azikwe na familia yake nchini Afrika Kusini, wakati Serikali ya Zambia iliutaka mwili wake kwa mazishi yanayofuata taratibu zote, ikiwamo ‘kupumzishwa’ katika makaburi rasmi ya viongozi mjini Lusaka.
Serikali ya Zambia ilikimbilia Mahakamani nchini Afrika Kusini na ndipo hukumu ilipotoka na kuipa haki ya kuchukua mwili kwa ajiri ya maziko.
Lakini, familia ya Lungu iligoma kukubaliana na hukumu hiyo, hivyo ikakata rufaa.
Hatimaye, Juni 23, 2026, familia ya Lungu ilishinda rufaa yake, hukumu inayowapa haki ya kuchukua mwili na kumzika kwa taratibu zao, pasi na kuihusisha Serikali.
Swali ni je; kwanini familia ya Lungu haikubaliani na kitendo cha Serikali ya Zambia kumzika gwiji huyo wa siasa?
Ziliwahi kuwapo taarifa kutoka katika familia, kwamba Lungu alisema Rais wa sasa, Hichilema, asihudhurie maziko wala kusogelea jeneza lake endapo ingetokea akafariki.
Kwanini? Kama tulivyoona katika sehemu zilizopita za makala haya, Lungu na Hichilema walikuwa washindani wakubwa wa nafasi ya urais katika siasa za Zambia.
Ukiweka kando Lungu kumpiku Hichilema katika chaguzi mbili (2015-2016 na 2016-2021), pia kulikuwa na sura nyingine ya uadui kati yao.
Kama itakumbukwa, tukio ambalo pia tuliliona katika sehemu zilizopita, Hichilema alisota gerezani kwa miezi minne baada ya Lungu kuingia madarakani katika Uchaguzi wa mwaka 2016.
Akikabiliwa na mashitaka ya uhaini, Hichilema alikuja kutoka gerezani baada ya kampeni nyingi za wanaharakati wa siasa na haki za binadamu wa ndani na nje ya nchi hiyo.
Tuliona pia, hata Hichilema alipoingia Ikulu mwaka 2021, Lungu naye alipitia nyakati ngumu mara kadhaa. Lipo tukio la polisi kuvamia nyumbani kwake na kupekua, kama tulivyokwishaona hapo awali.
Wakati huo, familia yake pia iliibuka na kusema Serikali ya Hichilema ilikuwa ikimuwekea vikwazo vya kwenda kwenye matibabu nje ya nchi.
Familia ikafichua pia, Lungu aliwahi kulazimika kusafiri kwa siri, akipita uwanja wa ndege bila kujulikana, ili kuhudhuria matibabu Afrika Kusini.
Swali ni je; Serikali ya Zambia itakubaliana na uamuzi wa sasa wa Mahakama kuipa ushindi familia ya Lungu au itakata rufaa?
Mwisho.


