DAKAR, Senegal
TAKWIMU zinaeleza kuwa asilimia 30 ya dawa za kulevya zinazokwenda Ulaya hupita barani Afrika, hasa katika mataifa ya Magharibi, ikiwamo Senegal.
Hiyo ni kwa mujibu wa utafiti wa Taasisi ya Kupambana na Uhalifu wa Kimataifa ya GI-TOC yenye Makao Makuu yake mjini Geneva, Uswis.
Katika ripoti yake, imeeleza kuwa wakati mashamba ya kilimo cha cocaine yakiwa kwa wingi Latin ya Amerika, soko kubwa liko Ulaya, huku Afrika Magharibi ikitumika kama njia ya kupitishia ‘mzigo’.
“Ukamataji (wa cocaine) umeongezeka maradufu tangu mwaka 2019 na kufikia tani takribani 30 kwa mwaka 2025,” imeeleza ripoti ya GI-TOC.
Ripoti hiyo inaeleza pia, kwamba boti moja ilikutwa ikiwa na tani 10, kiwango kikubwa zaidi cha cocaine kuwahi kubebwa na kifaa hicho cha usafiri wa majini.
Aidha, vitendo vya rushwa katika baadhi ya nchi za Afrika ya Magharibi vinawavutia wasafirishaji wa cocaine kutumia njia hiyo, kuliko kwenda moja kwa moja (kutoka Amerika ya Latin hadi Ulaya).
Lucia Bird ni mwandishi wa Ripoti ya GI-TOC. Anafafanua hilo la rushwa akisema: “Katika baadhi ya nchi, wahusika ni wanasiasa, na wakati mwingine ni wale wenye mamlaka makubwa katika nchi. Kwa nchi zingine, ni maofisa wanaofanya kazi katika bandari au viwanja vya ndege.”
Anaeleza kuwa faida itakanayo na biashara ya cocaine inaongezeka kwa kasi duniani, hivyo kuzidi kuongeza dau la rushwa na kufanya vita dhidi ya dawa hizo izidi kuwa ngumu.
“Soko la cocaine limekuwa chanzo kizuri cha mapato kwa watumishi wa umma na wanasiasa wakubwa Afrika Magharibi,” amesema Lucia.
Tangu mwaka 2021, zimekuwapo kashfa nyingi za mawaziri nchini Guinea-Bissau kuhusishwa na biashara ya cocaine. Januari, 2025, begi la Balozi wa Sierra Leone nchini humo lilikutwa kwenye gari likiwa na dawa hizo.
Kwa upande mwingine, wakati Afrika ya Magharibi ikitafsiriwa kama njia, pia utumiaji wa cocaine nao unatajwa kuongezeka miongoni mwa vijana wa nchi za Ukanda huo, ikiwamo Senegal.
“Si tu njia ya kupeleka Ulaya. Pia, (Afrika Magharibi) inatumika kuhifadhi, kufunga na kusambaza cocaine,” amesema Mouhamadou Kane, ambaye pia ni mwandishi wa Ripoti hiyo.


