Na mwandishi wetu, Gazetini
MFUKO wa Barabara (RFB) umesema tozo zinazotozwa kwenye mafuta ya petroli na dizeli ndizo chanzo kikuu cha fedha zinazowezesha matengenezo ya barabara nchini, hatua inayosaidia kuhakikisha miundombinu hiyo inaendelea kuwa salama na kupitika wakati wote.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa RFB, Mhandisi Rashid Kalimbaga, amebainisha hayo leo Jumamosi Juni 20, 2026 wakati akitoa elimu kwa wananchi waliotembelea banda la taasisi hiyo katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2026 yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma.
Amesema kupitia mapato yanayotokana na tozo za mafuta pamoja na tozo za magari ya kigeni yanayotumia barabara za Tanzania, Mfuko wa Barabara kwa sasa unafadhili matengenezo ya mtandao wa barabara wenye zaidi ya kilomita 181,000 nchini.
“Kila mchango unaotokana na tozo za mafuta una nafasi muhimu katika kuhakikisha barabara zinaendelea kuwa salama na zenye ubora,” amesema Mhandisi Kalimbaga.
Ameongeza kuwa wananchi wanapaswa kufahamu kuwa michango inayotokana na matumizi ya mafuta ina mchango wa moja kwa moja katika kuboresha miundombinu ya usafiri na usafirishaji, ambayo ni muhimu kwa ukuaji wa uchumi na utoaji wa huduma za kijamii nchini.


