Na Hassan Mwasha, Gazetini
KASI kubwa ya maendeleo imeshuhudiwa katika bandari za mwambao wa Bahari ya Hindi na Maziwa Makuu, ikiwamo uboreshaji wa miundombinu unaochagiza utoaji wa huduma unaokidhi viwango vya kitaifa na kimataifa.
Katika kipindi cha Julai, 2025 hadi Machi 2026, Wizara ya Uchukuzi kupitia Mamlaka ya Bandari nchini (TPA), ilihudumia jumla ya tani milioni 29.66 za shehena, sawa na ongezeko la asilimia 27.96, ikilinganishwa na tani milioni 23.18 zilizohudumiwa katika kipindi kama hicho cha mwaka wa fedha uliopita (2024/25).
Aidha, shehena iliyosafirishwa kwenda nchi jirani imeongezeka hadi kufikia tani milioni 10.93, ikilinganishwa na tani milioni 8.24 zilizohudumiwa katika kipindi kama hicho kwa mwaka wa fedha 2024/25, sawa na ongezeko la asilimia 32.64.
Akiwasilisha Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2026-27 jana Mei 13, 2026, Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amesema ongezeko hilo limetokana na uboreshaji wa miundombinu na ushirikishwaji wa sekta binafsi.
MWAROBAINI CHANGAMOTO YA UHIFADHI WA MAFUTA
Katika hotuba yake Bungeni mjini Dodoma, Waziri Mbarawa alieleza pia Serikali ya Awamu ya Sita ilivyoweka mikakati ya kukabiliana na chagamoto sugu ya uhifadhi wa mafuta.
“Serikali ya Awamu ya Sita imeamua kulifanyia kazi suala hilo kwa vitendo, ambapo TPA imeanza ujenzi wa miundombinu ya kupokelea na kuhifadhi mafuta (Single Receiving Terminal – SRT) unaohusisha ujenzi wa matenki 15 ya mafuta (tank farms) yenye uwezo wa kuhifadhi mita za ujazo 378,000, ambapo utekelezaji umefikia asilimia 42 na unatarajiwa kukamilika mwezi Agosti, 2026,” alisema.
UJENZI WA BANDARI YA BAGAMOYO
Kwa upande mwingine, katika kutanua huduma za bandari nchini, Waziri Mbarawa alifichua pia Serikali kupitia TPA iko mbioni kukamilisha maandalizi ya kuanza utekelezaji wa mradi huo wa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo.
“Bandari hiyo itahusisha ujenzi wa gati lenye urefu wa kilomita 1.32 pamoja na miundombinu wezeshi ya kuhudumia meli kubwa za kisasa aina za Megamax ambazo haziwezi kuhudumiwa katika Bandari ya Dar es Salaam kwa sasa.
“Katika kutekeleza awamu ya kwanza ya Mradi huo, tayari mitambo kwa ajili ya uchimbaji wa kina cha maji imepatikana na kazi hiyo inatarajiwa kuanza rasmi katika mwaka wa fedha 2026/27,” amesema.
UFUMBUZI MSONGAMANO BANDARI YA DAR
Ili kukabiliana na msongamano katika Bandari ya Dar es Salaam, matumizi ya bandari kavu nchini, ikiwemo Bandari Kavu ya Kwala iliyopo Mkoa wa Pwani, yamekuwa na mchango mkubwa.
“Kufikia mwezi Machi, 2026 bandari hiyo ilihudumia makasha 14,460. Katika hatua nyingine, mwezi Machi, 2026 TRC ilianza usafirishaji wa shehena kwenda katika Bandari Kavu ya Isaka,” amesema.

KASI KUBWA YA UBORESHAJI, USHIRIKI WA SEKTA BINAFSI
Katika hatua nyingine, Waziri Mbarawa ameainisha maboresho makubwa yaliyofanyika katika bandari za Maziwa Makuu, ambapo hadi kufikia mwezi Machi, 2026 uboreshaji wa Bandari za Bukoba na Kemondo ulikamilika.
“Uboreshaji wa Bandari ya Mwanza North umefikia asilimia 75. Serikali inaendelea na Mradi wa Uboreshaji wa Bandari ya Kigoma ambao umefikia asilimia 13. Kwa upande wa bandari ya Mbamba Bay umefikia asilimia 49,” amesema.
Juu ya ushirikishwaji wa sekta binafsi katika shughuli za uendelezaji na uendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam, Waziri Mbarawa amesema hatua hiyo imekuwa na tija kubwa kwani imeongeza ufanisi na ushindani katika utoaji wa huduma za kibandari nchini.
Baadhi ya mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kuongezeka kwa shehena inayohudumiwa katika Bandari ya Dar es Salaam kutoka tani milioni 16.27 mwaka wa fedha 2020/21 hadi kufikia tani milioni 27.76 mwaka 2024/25, sawa na ongezeko la asilimia 70.62.
Aidha, pia ushirikishwaji wa sekta binafsi umepunguza gharama za uendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam kutoka Sh bilioni 652.83 mwaka 2023/24 hadi Sh bilioni 308.95 mwaka 2024/25.
Kama hiyo haitoshi, kumekuwapo na ongezeko la makusanyo ya mapato ya TPA yatokanayo na ada za huduma za kibandari kutoka Sh bilioni 896.95 mwaka 2020/21 hadi kufikia Sh trilioni 1.30 mwaka 2024/25.
“Vilevile, ni kupungua kwa muda wa kuhudumia meli za makasha gatini kutoka wastani wa siku 10 hadi siku 3 na kpungua kwa muda wa meli kusubiri nangani kutoka wastani wa siku 46 hadi wastani wa siku 7 kwa meli za mizigo mchanganyiko na kichele,” amesema.
MIKAKATI ZAIDI, UJENZI WA SGR MBIONI KUKAMILIKA
Katika hotuba yake, Waziri Mbarawa amesema utekelezaji wa ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR inayoingia moja kwa moja bandarini (Port Link) umefikia asilimia 99.7 na majaribio ya usafirishaji wa mizigo kwa njia hiyo yanaendelea.
Pia, kuna ujenzi unaoendelea wa eneo maalum (loading platform) la kupakilia mizigo kwenye treni za SGR ndani ya eneo la bandari kwa lengo la kuongeza kasi, na ufanisi katika utowaji wa mizigo.
Mkakati mwingine ni kuendelea na upanuzi wa eneo la Kurasini lenye ukubwa wa mita za mraba 220,000 kwa ajili ya kuhudumia makasha 700,000 kwa mwaka.
“Awamu ya kwanza ya mradi huo inatarajiwa kukamilika mwezi Juni 2026 na kuhudumia makasha 150,000 kwa mwaka, huku Awamu ya Pili ikitarajiwa kukamilika mwezi Julai 2027,” amesema Waziri Mbarawa.
Wakati huo huo, mkakati mwingine ni kujenga kituo cha kisasa cha mizigo katika Stesheni ya SGR Morogoro chenye ukubwa wa mita za mraba 68,000 na uwezo wa kuhudumia makasha 600 kwa siku, kwa ajili ya kuhudumia mizigo inayosafirishwa kwa njia ya barabara kuelekea mikoa mbalimbali na nchi za jirani.


