16.5 C
New York

Watoto 75,500 nchini kuchunguzwa Sikoseli

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

JUMLA ya watoto na vijana wapatao 75,500 wanatarajiwa kufanyiwa uchunguzi wa ugonjwa wa selimundu (sikoseli) ili kubaini mapema hali zao za kiafya na kuwapatia huduma stahiki, kupitia mradi wa miaka mitatu unaotekelezwa kwa pamoja nchini Tanzania na Kenya.

Kwa mujibu wa taarifa ya mradi huo, watoto wachanga 45,000 watafanyiwa uchunguzi, huku watoto wenye umri chini ya miaka mitano wakiwa 12,500 na vijana 18,000.

Akizungumza Aprili 23, 2026 kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Serikali katika uzinduzi wa mradi huo, Dk. Gunini Kamba, amesema bado kuna changamoto ya kuwabaini mapema watoto na vijana wenye sikoseli, hali inayochangia kuchelewa kwa huduma muhimu.

“Utekelezaji wa mradi huu utawezesha kuibua mapema watoto na vijana wenye ugonjwa huu na kuwapatia huduma muhimu zinazohitajika kwa wakati,” amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wataalamu wanaopambana na sikoseli nchini, Dk. Elisha Osati, amesema kati ya asilimia 15 hadi 20 ya Watanzania wanaishi na vinasaba vya ugonjwa huo, huku vifo vya watoto chini ya miaka mitano vinavyotokana na sikoseli vikikadiriwa kufikia asilimia 5 hadi 7.

Naye shujaa wa sikoseli, Samweli Maingu, amesema changamoto za ugonjwa huo ni nyingi, ikiwamo maumivu makali na upatikanaji wa huduma.

“Sikoseli ni ugonjwa unaoumiza na kutesa sana, hivyo ni muhimu kwa jamii kujitambua kiafya kwa kupima mapema ili kusaidia kupunguza kasi ya ugonjwa huu nchini,” amesema.

Mradi huo wa SCD KenTan unalenga kupunguza athari za ugonjwa wa sikoseli kwa watoto na jamii kwa kuboresha uchunguzi wa mapema, utambuzi sahihi na huduma jumuishi kwa waathirika pamoja na walezi wao.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img