Na mwandishi wetu, Gazetini
BAADA ya Yanga kuanza kwa ushindi msimu huu wa Ligi Kuu Bara (2026-27), Simba nayo imejibu mapigo kwa kuitandika Kagera Sugar mabao 2-0.
Simba ikiwa ugenini katika Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba leo Agosti 16, 2026, imepata ushindi huo kwa mabao ya beki Olivier Toure (Dk. 45) na mshambuliaji Elie Mpanzu (Dk. 71).
Kwa upande wao, Yanga ambao ndiyo mabingwa watetezi, nao walikuwa ugenini jana na kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Namungo.
Kwa matokeo hayo, kila moja imefikisha pointi tatu, ambapo Yanga iko nafasi ya pili, ikifuatiwa na Simba, huku Singida Black Stars ikiwa kileleni kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Hata hivyo, msimamo huo wa Ligi msimu huu wa 2026-27 ni kabla ya mechi nyingine ya leo kati ya JKT Tanzania na TRA United.


