Na mwandishi wetu, Gazetini
TAARIFA ya Dawa za Kulevya ya Dunia ya mwaka 2025 inaonesha kuwa matumizi ya dawa za kulevya katika umri mdogo yana madhara makubwa, yanayopelekea vifo, pamoja na changamoto za kiafya na kijamii.
Vijana hutumia dawa za kulevya kwa kiwango kinachofanana au kuzidi watu wazima, hususani wanafunzi wa shule za sekondari wenye umri wa miaka 15 na 16 kuliko ilivyo kwa idadi ya watu wazima.
Nchini Guinea, asilimia 0.94 ya wanafunzi waliohojiwa waliripoti kutumia ‘kush’ na kuifanya kuwa dawa ya tatu kwa matumizi baada ya bangi na viyeyushi (inhalants).
Katika eneo la Oceania (Australia, Visiwa vya Pasifiki na New Zealand), matumizi ya bangi miongoni mwa wanafunzi wa miaka 15 na 16 ni asilimia 13, kiwango ambacho ni cha juu zaidi, ikilinganishwa na wastani wa dunia wa asilimia 4.4.
Barani Ulaya, matumizi ya bangi miongoni mwa vijana wa miaka 15 na 16 bado yako juu zaidi kuliko watu wenye umri wa miaka 15 hadi 64.
Tafiti zinaonesha kuwa, matumizi ya bangi katika kipindi cha ujana yanaweza kuathiri uwezo wa kufikiri, kuvuruga maendeleo ya kitaaluma na binafsi, na kupunguza ufanisi katika masomo pamoja na fursa za ajira baadaye maishani.
Matumizi ya mara kwa mara, hasa yanapoanza katika umri mdogo, yanaweza pia kuongeza hatari ya kuchanganyikiwa, matatizo ya hisia na wasiwasi, hali inayoathiri ukuaji na maendeleo.
Taarifa ya Dawa za Kulevya ya Dunia ya mwaka 2025 inaeleza kuwa sababu zinazochochea matumizi ya dawa za kulevya miongoni mwa vijana ni malezi duni, kutelekezwa utotoni, urahisi wa upatikanaji wa dawa na sababu binafsi.
Hivyo, juhudi za kinga huwa na ufanisi zaidi zinapolenga kushughulikia sababu za mtu binafsi pamoja na mazingira kwa mapana, hususan katika familia na shule.


