Na mwandishi wetu, Gazetini
TAARIFA ya hali ya Dawa za Kulevya Duniani ya mwaka 2025 ilionesha kuwa matumizi ya dawa za kulevya yamefikia kiwango cha juu zaidi kuwahi kurekodiwa katika historia.
Taarifa hiyo inaonesha kuwa kiwango cha matumizi ya dawa za kulevya kimeendelea kuwa juu zaidi katika eneo la Amerika Kaskazini, ikilinganishwa na maeneo mengine duniani.
Aidha, taarifa hiyo inabainisha kuwa, watu wapatao milioni 316 duniani, wenye umri wa miaka 15 hadi 64, walitumia angalau aina moja ya dawa za kulevya katika mwaka 2023.
Hii ni sawa na takribani asilimia 6 ya watu wote duniani, ikiwa ni ongezeko la asilimia 28 la matumizi ya dawa za kulevya, ikilinganishwa na miaka 10 iliyopita. Moja ya sababu ya ongezeko hili linatokana na kuongezeka kwa idadi ya watu duniani.
Mwaka 2023, bangi iliendelea kuwa dawa ya kulevya inayotumika zaidi duniani, ambapo watu milioni 244 (4.6% ya watu wenye umri wa miaka 15 hadi 64) waliripoti kuitumia ndani ya kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Miongoni mwa sababu zinazochangia ongezeko hili ni kuhalalishwa kisheria kwa matumizi ya bangi kwa madhumuni yasiyo ya kitabibu katika baadhi ya nchi, zikiwemo Canada, Uruguay, Malta, Luxembourg, Ujerumani na Afrika Kusini.
Dawa zilizofuata kwa wingi wa matumizi ni dawa za kulevya jamii ya afyuni zikitumiwa na watu milioni 61 (1.2%), jamii ya amphetamine zilitumiwa na watu milioni 31 (0.6%), Cocaine zenye watu milioni 25 (0.5%), na ‘ecstasy’ yenye watumiaji milioni 21 (0.4%).
Aidha, taarifa hiyo ilionesha kuwa ongezeko la matumizi ya dawa za kulevya yameendelea kuleta madhara makubwa kiafya, kijamii na kiuchumi.
Katika ripoti hiyo, inakadiriwa kuwa mwaka 2021, matumizi hayo yalipelekea vifo vya takribani watu milioni 28.
Matumizi ya dawa za kulevya kwa njia ya kujidunga yameendelea kuchochea maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) na vile vya homa ya ini aina ya B na C.
Kwa mjibu wa taarifa hiyo, watu wapatao milioni 14 duniani walitumia dawa za kulevya kwa njia ya kujidunga.
Kati yao, milioni 1.7 walikutwa na maambukizi ya VVU, milioni 6.9 walikuwa na homa ya ini aina C na milioni 1.5 walikuwa na yote mawili (VVU na homa ya ini aina C).


