Na mwandishi wetu, Gazetini
NAIBU Waziri wa Nishati, Salome Makamba amesema wananchi wa Mkoa wa Rukwa wataanza kupata umeme wa gridi kuanzia mwezi mei mwaka huu mara utakapokamilika mradi wa usafirishaji umeme wa msongo wa kV 400 kutokea mkoani Iringa.
Ameyasema hayo katika Mji wa Laela, Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga wakati wa ziara ya Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba iliyoanza jana mkoani Rukwa.
“Kwa maelekezo ya Rais, Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan na kwa maelekezo yako pia,, tunaendelea kuhakikisha inapofika mei 2026 tunawasha umeme kupitia mradi wa TAZA. Hali ya mradi inaenda vizuri na kama kila kitu kitakwenda kama kilivyo, itakapofika mwezi wa tano mwaka huu hatimaye Mkoa huu wa Rukwa utanufaika na umeme wa gridi,” amesema Salome.
Ameeleza kuwa, kwa sasa mkoa wa Rukwa unapata umeme kutoka nchini Zambia kupitia mashirikiano ya biashara ya umeme katika nchi za Ukanda wa Kusini mwa Afrika (Southern Africa Power Pool) ambayo yanawezesha nchi wanachama kuuza au kununua umeme pale kunapokuwa na uhitaji ili kukidhi mahitaji ya wananchi.
Ameongeza kuwa, kutokana na nchi kuwa na umeme wa kutosha, kazi zinazoendelea ili kuweza kuutumia umeme huo ipasavyo ni ujenzi wa miundombinu imara ya usafirishaji na usambazaji umeme itakayowezesha kufikisha huduma hiyo kwa wananchi wengi.
Kuhusu Nishati Safi ya Kupikia, amesema jitihada mbalimbali zinaendelea ili kuweza kufikia asilimia 80 ya wananchi wanaotumia Nishati Safi ya Kupikia ifikapo 2034 ikiwemo ya kusambaza majiko banifu na mitungi ya gesi kwa bei ya ruzuku.


