9.5 C
New York

Mwangwi wa sheria| Mambo usiyoyajua kisheria kuhusu kesi za mauaji-2

Published:

Na Wakili Baraka Asajile Gwakabale

KIFUNGU cha 196 kinaweka msingi wa kosa la murder. Lakini kifungu cha 203 ndicho kinachoeleza kwa kina uwiano wa sababu kati ya kitendo cha mshtakiwa na kifo kilichotokea. Mahakama haitoshi kusema kulikuwa na ugomvi na baadaye mtu akafa. Hilo ni hadithi, si ushahidi.

Kisheria, upande wa mashtaka lazima uthibitishe mambo matatu kwa mpangilio usiokatika.

Kwanza, kuwa mshtakiwa alifanya kitendo fulani. Pili, kuwa kitendo hicho kilikuwa hatarishi au cha jinai. Tatu, kuwa kifo kilichotokea ni matokeo ya moja kwa moja ya kitendo hicho bila sababu mpya kujitokeza katikati.

Huu ndio unaoitwa mlolongo wa sababu (chain of causation). Ukikatika mahali popote, murder haiwezi kusimama.

Kwa mfano, kama jeraha lilitokea lakini kifo kikaja baadaye kwa sababu nyingine isiyohusiana moja kwa moja, mahakama lazima ichambue kwa makini iwapo uwajibikaji bado unamhusu mshtakiwa. Hapa ndipo ushahidi wa kitabibu unapata uzito mkubwa.

Mahakama huuliza; je, bila kitendo cha mshtakiwa, kifo kingetokea? Je, kulikuwa na tukio jipya lililokatiza mlolongo wa sababu? Je, kifo kilikuwa matokeo yanayotabirika ya kitendo hicho? Bila majibu ya wazi, hakuna murder.

Ifahamike pia, murder na ‘manslaughter’ si kosa moja. Vifungu husika hapa ni vya 195 na 196 vya Penal Code, Cap 16.

Hili ni eneo ambalo hata wasomi wa sheria hulichanganya kama hawako makini. Kisheria, kila kifo kinachosababishwa na mtu si murder. Sheria imeweka mipaka wazi.

Kifungu cha 195 kinatambua kosa la manslaughter, wakati kifungu cha 196 kinahusu murder. Tofauti yao si tukio, ni hali ya akili ya mtuhumiwa wakati kitendo kinatokea.

Murder inasimama pale ambapo upande wa mashtaka unathibitisha kulikuwa na nia ovu, nia hiyo ilikuwa ya kuua au kusababisha madhara makubwa na kifo kilikuwa matokeo ya kitendo hicho.

Manslaughter, kwa upande mwingine, hutokea pale ambapo kifo kimetokea, kitendo kilikuwa batili au cha uzembe, lakini hakukuwa na nia ovu kama inavyotakiwa katika murder.

Hapa ndipo sheria inaonyesha busara yake. Kwamba mtu anaweza kusababisha kifo kwa hasira ya ghafla, kwa uzembe, kwa kujitetea lakini akazidisha nguvu, au kwa mazingira yasiyokuwa na mipango ya awali.

Katika hali hizo, sheria haisemi mtu huyo hana kosa. Inasema kosa lake si murder, bali manslaughter.

Mahakama hutazama kwa makini muda wa tukio, chanzo cha mgogoro, kiwango cha nguvu kilichotumika, na kama kulikuwa na nafasi ya kutafakari kabla ya kitendo.

Kama nia nzito ya jinai haijathibitishwa, murder huanguka moja kwa moja, hata kama matokeo ni kifo.

Itaendelea…Mawasiliano: – 0784745645

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img